Ujue mtambo wa biogesi bana matumizi Tanzania

Na Rodgers George
2 Oct 2021
Ukiununua mtambo huo kazi yako ni kuulisha taka zinazooza hadi kilo 15 ambazo zitakuwezesha kupika hadi Saa 4.
article

Dar es Salaam. Ni kawaida katika nyumba yeyote kuwa na takataka mbalimbali zikiwemo zinazotokana na vyakula na makaratasi. 

Pamoja na kaya kuwa na taka hizo, si wote wanafahamu kuwa uchafu huo ni mali. Taka ambazo haziozi kama karatasi zinaweza kutumika kwenye shughuli za urejereaji na kutengeneza bidhaa nzuri yakiwemo maboksi na mkaa mbadala usiochafua mazingira. 

Kwa taka zinazooza, kidogo kumekuwa na changamoto ya namna ya kuzitumia vema badala ya kuishia kuzitupa.

Changamoto huanzia pale utupwaji wake unapokuwa sio mzuri na hivyo kusababisha harufu mbaya na saa zingine wadudu kama funza na nzi kuwa sehemu ya nyumba yako. 

Hata hivyo, huenda changamoto hiyo ikasahaulika baada ya wataalamu wa teknolojia kubuni  mtambo wa kufua biogesi baada ya kujazwa hadi kilo 15 za taka kwa siku.

Mtambo huo, unaotengenezwa na kampuni ya wazawa ya Ichi Renewable Energies, una ukubwa wa mita 2.5 kwa 2.5 au sawa na mita za mraba 6.25. 

Ni nini kipya?

Mtambo huo unaotumika kuzalisha nishati ya gesi ambayo inaweza kutumika nyumbani kwa ajili ya kupikia na kuwasha taa.

Mkurugenzi wa Ichi Energies, Iqualiptus Malle ameiambia Jiko Point (jikopoint.co.tz) kuwa mtambo huo pia unaweza kuzalisha mbolea kwa ajili ya mimea na kuwasaidia wakulima na maumivu ya uhaba wa mbolea. 

Mtaalamu huyo anasema mtambo huo baada ya kujazwa taka za lita 15 kwa siku unaweza kuzalisha gesi ya kupikia kwa saa nne kwenye jiko moja. Taka hizo ni taka za jikoni na kwa mitambo mikubwa zaidi, hata kinyesi cha binadamu na wanyama kinaweza kutumika. 

Mtambo huo unaweza kuzalisha nishati ya kupikia kwa hadi Saa 4 kwa siku zinazoweza kupikia chai, chakula cha mchana na chakula cha jioni. Picha| Ichi Renewable Energies.

Mtaji ni takataka

Tofauti na mitungi ya gesi ambayo mtumiaji hutakiwa kujaza kila unapoisha, mtambo huu wa biogesi mtaji ni kuulisha taka taka kila siku ili kupata gesi ya kutosha kupikia. 

“Malighafi ya kutengeneza mtambo huo ni maalumu na tenki linaweza kudumu kwa zaidi ya miaka mitano likiwa limewekwa juani na likiwa kivulini, linaweza kudumu zaidi ya miaka nane,” amesema Malle.

Mtambo huu unaweza kusaidia kuondoa kero ya taka nyumbani pamoja na kupunguza matumizi ya mkaa kwa kuwa na gesi ya kupikia ambayo ni moja ya nishati safi zinazosaidia kuokoa mazingira kwa kupunguza hewa ukaa.

Kuupata mtambo huu unahitaji Sh990,000 ambayo kwa mujibu wa Malle, fedha hiyo ni gharama ya mtambo pekee. Kuna gharama zingine ikiwemo ufungaji na usafirishaji ambazo Malle amesema zinahimilika.

Mtambo huu kwa sasa mbali na kufika dukani kwao, unaweza kuununua Jiko Sokoni au  www.jikopoint.co.tz au jikosokoni.co.tz

Kwa wenye hoteli na maeneo makubwa, ipo mitambo ya namna mbalimbali inayofikia hadi Sh54 milioni ikiwa na ukubwa wa mita 5.0 kwa mita 15 ambao uwezo wake ni kumpatia mtumiaji gesi ya kutosha kutumika kwa saa 90 kwenye sahani mbili za jiko.

Ubunifu na matumizi ya nishati yamezidi kuongezeka siku za hivi karibuni nchini Tanzania kiasi kinachochangia kupunguza uchafuzi wa mazingira na maradhi yatokanayo na kutumia kuni na mkaa ukiwemo ugonjwa kifua na macho. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa