Jinsi unavyoweza kupika keki ya vanilla nyumbani

Na Fatuma Hussein
3 Jan 2024
Ukiweza kutengeneza aina hii basi nyingine zote utajifunza bila shida yoyote.
article
  • Unaweza kujifunza kwa ajili ya biashara au kwa ajili ya familia.
  • Utahitaji ‘oven’ au jiko la mkaa ili kuivisha keki kwa urahisi nyumbani.

Unaonaje ukianza mwaka mpya na ujuzi wa mapishi ya keki ambayo unaweza kuwapikia uwapendao au ikawa miongoni mwa vyanzo vyako vya ‘maokoto’.

Ndio! mwaka huu usikae kizembe, tumekusogezea kiganjani mwako maujanja ya kuandaa keki ambayo ni sehemu ya matukio muhimu kama sherehe za kuzaliwa harusi na nyinginezo.

Nikufahamishe tu kipande kimoja cha keki hii huuzwa kuanzia Sh500 hadi Sh5,000 kutegemea na aina ya ladha uliyoweka na ukubwa, hivyo hii sio mishe ya kitoto.

Katika aina nyingi ya keki zilizopo duniani leo tutajifunza kuandaa aina rahisi zaidi ambayo ni keki ya vanilla, ukiweza kutengeneza aina hii basi nyingine zote utajifunza bila shida yoyote.

Haya sasa karibu tujifunze kwa pamoja 

Wakati tunasogelea jiko nikukumbushe tu keki hii tunapika nyumbani hivyo mahitaji yote ni yale yanayopatikana kwa urahisi nyumbani au dukani.

Kwa kuanza tutaandaa unga wa ngano, hakikisha  umepata unga wa keki au maandazi na kuuchekecha ili kuondoa uchafu wowote unaoweza kuwepo.

Katika bakuli lingine andaa bakuli safi weka sukari kiasi kulingana na uhitaji wako, kwa unga robo unaweza kutumia robo kikombe cha chai, weka siagi gramu 125 kisha koroga na mwiko au mchapo mpaka sukari ichanganyike kabisa.

Kama una mchapo au mashine ya kuchanganyia (hand mixer) inaweza kurahisisha hatua hii, baada ya hapo ongeza yai moja moja katika bakuli lako huku ukikoroga mpaka mayai manne yaishe.

Kwa unga  robo unaweza kutumia mayai manne mpaka matano na kadri utakavyoongeza unga ndivyo utakavyoongeza mayai.

Hatua hiyo ikikamilika ongeza maziwa kiasi na kama huna basi ongeza maji nusu kikombe cha chai, umimine unga taratibu huku ukikoroga mpaka pale utakapoisha na kama unga ukiwa mwingi basi ruksa kuongeza maji taratibu taratibu.

Hakikisha mchanganyiko wako si mzito sana wala si mwepesi kisha ongeza vannila yako kijiko kimoja na ufunike tayari kwa kuhamishia jikoni.

Ukifika hatua ya kuoka chaguo ni lako, unaweza kutumia ‘oven’ au jiko la mkaa ambalo litakufanya upike kwa muda mrefu zaidi.

Kupika keki kwa kutumia sufuria mbili hupunguza uwezekno wa kake yako kuungua na kuifanya iive vizuri.Picha|Bakingo.

Kama unatumia oven basi eka moto wa 240 kwa dakika 30 hadi 40 kisha mimina mchanganyiko wako katika chombo maalum cha kuoka na uache iive.

Kwa jiko la mkaa, anza kwa kuliwasha mpaka likolee kabisa, punguza makaa kisha bandika kubwa ambayo utalazimika kutanguliza mchanga ndani ya sufuria na ukipata moto ndipo uweke sufuria nyingine au chombo cha kuoka keki ambacho umeweka mchanganyiko wako.

Tafuta mfuniko utakaotosha kufunika sufuria zote mbili kisha upalie makaa katika mfuniko wa sufuria kubwa na usubiri kwa dakika 45 au zazidi ili keki iive.

Tumia kijiti kikavu au kisu kuchoma keki yako Kabla ya kuepua ili kuhakikisha keki yako kama imeiva.kijiti kikitoka kikavu basi itakuwa tayari kwa kula.

Usikose kufatilia makala ijayo ya upishi wa keki, ambapo tutaangazia mbinu zaidi za kupika keki tamu iliyochambuka.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa