Jinsi ya Kutengeneza mvinyo wa machungwa

Na Fatuma Hussein
9 Sept 2024
Kwa waliozoea kutumia machungwa kama tunda au kama juisi ya kawaida wanaweza wasiamini kuwa tunda hilo linaweza kutengeneza mvinyo, wenye uwezo wa kuwaburudisha wanywaji. Kwa mujibu wa kitabu cha matunda na mboga mboga kinachotolewa na Wizara ya Kilimo aina hii ya mvinyo ina wingi wa virutubisho ikiwemo sodiamu, potasiamu, kalsiamu na fosforasi. Kinywaji hiki pia […]
article
  • Funika chombo chako kwa kutumia kitanzi cha hewa kwa siku 21.
  • Unaweza kuuacha mvinyo ukae kwa muda mrefu zaidi

Kwa waliozoea kutumia machungwa kama tunda au kama juisi ya kawaida wanaweza wasiamini kuwa tunda hilo linaweza kutengeneza mvinyo, wenye uwezo wa kuwaburudisha wanywaji.

Kwa mujibu wa kitabu cha matunda na mboga mboga kinachotolewa na Wizara ya Kilimo aina hii ya mvinyo ina wingi wa virutubisho ikiwemo sodiamu, potasiamu, kalsiamu na fosforasi.

Kinywaji hiki pia kina kileo cha asilimia 10 hadi 12 hivyo hakifai kutumiwa na watoto, wazee, wagonjwa hususani wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo, kisukari na presha.

Kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wananweza kutumia mwongozo wa kutengeneza kinywaji hiki uliotolewa na Wizara ya Kilimo kujiongezea kipato.

Hatua za Kufuata 

Hatua ya kwanza chagua machungwa yaliyoiva vizuri na yasiyoshambuliwa na wadudu. Yasafishe kwa maji safi na salama, kisha menya ili kuondoa maganda. 

Baada ya kumenya, kamua machungwa kupata lita 10 za  juisi safi safi ya machungwa kisha uondoe mabaki na mbegu kwa kutumia chujio na uchanganye juisi hiyo na lita 30 za maji.

Baada ya hapo hatua inayofuata ni kuchemsha mchanganyiko wa juisi na maji kwa dakika 30 kwenye moto wa wastani, huku ukikoroga mara kwa mara. Ongeza sukari na koroga hadi iyeyuke kabisa baada ya hapo, acha mchanganyiko huo upoe hadi kufikia nyuzi joto 30 za Sentigredi.

Baada ya mchanganyiko kupoa, ongeza hamira ya mvinyo na koroga vizuri kisha uache mchanganyiko huo uumuke wakati huo endelea kuandaa chai kwa kuchemsha majani ya chai gramu 200 na lita moja ya maji mpaka ibaki nusu lita. Chuja chai hiyo na uache ipoe.

Hatua inayofuata changanya mchanganyiko wa juisi, chai iliyochemshwa, na hamira iliyoumuka.Weka mchanganyiko huo kwenye chombo cha kuchachulia.

Baada ya hapo funika chombo chako kwa kutumia kitanzi cha hewa (air lock) ili kuruhusu hewa kutoka bila kuingia ndani kwa muda wa siku 21.

Baada ya siku 21,hewa ikikoma kutoka, chuja mvinyo na tenga masimbi. Weka maji kwenye masimbi na uache yatoke hewa kwa wiki moja zaidi,kisha chuja tena kupata mvinyo safi, rudia hatua hii mara mbili au tatu ili kuhakikisha unapata mvinyo ulio safi kabisa.

Hatua nyingine ni kuchuja vizuri, weka mvinyo kwenye chombo kisichopitisha hewa. Pima kiwango cha kileo, ambapo kinatakiwa kufikia asilimia 12 au zaidi na fungasha mvinyo kwenye chupa zenye vifuniko visivyopitisha hewa.

Mpaka hapo mvinyo wako utakuwa tayari ila unaweza kuuweka kwa muda mrefu zaidi ili uwe bora na ladha inayovutia zaidi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa