Kutana na jiko la umeme linalookoa gharama za mapishi

Na Daniel Samson
18 Nov 2022
Muundo wa jiko hilo humuwezesha mmiliki kutumia umeme mchache tofauti na anayetumia jiko la kawaida la umeme kupikia.
article

  • Linatumia joto kuivisha chakula.
  • Lina uwezo kupika vyakula vya aina zote kwa umeme kidogo.
  • Ni suluhu ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa. 

Takriban watu bilioni 3 duniani kote hawana uwezo wa kupata teknolojia ya kisasa ya kupikia na badala yake wanategemea kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia, jambo linalowaweka katika hatari ya kuendelea kuathirika na nishati hizo. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, inakadiriwa kuwa watu 33,000 nchini Tanzania wanafariki dunia kila mwaka kutokana na kuvuta sumu za moshi unaotoka kwenye kuni na mkaa wakati wa kupika. 

Mbali na athari za kiafya ambazo zinachangia uwepo wa zaidi ya theluthi mbili ama asilimia 70 za magonjwa ya upumuaji, matumizi ya nishati zisizo safi yanachangia ongezeko la hewa ya ukaa inayochafua mazingira na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linaeleza kuwa takriban vifo milioni 4 vya mapema vinavyotokana na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba vinahusishwa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia hutokea duniani kote kila mwaka.

Kukabiliana na athari hizo wadau wa mazingira na wabunifu wameendelea kubuni teknolojia rahisi za kupikia majumbani ili kuwawezesha watu hasa wanawake kutumia nishati safi na salama ya kuboresha maisha yao. 

Miongoni mwa teknolojia hizo ni matumizi ya majiko yanayotumia kiasi kidogo cha umeme (electric pressure cookers (EPCs)). Majiko hayo licha ya kuwa bado hayatumiki sana kwenye jamii kutokana na uelewa mdogo lakini yameonyesha ufanisi mzuri wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Jiko la umeme la Sescom lina uwezo mkubwa kwa kupika vyakula vingi kwa umeme kidogo. Picha| Sescom.

Nchini Tanzania, majiko hayo yamekuwa yakizalishwa na kampuni ya huduma za nishati endelevu (Sescom) iliyo chini ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi ya Mazingira (Tatedo). 

Majiko hayo hayatumii umeme moja kwa moja. Yameundwa kufanya kazi kwa kutumia shinikizo la joto (pressure) inayotengenezwa na umeme wa gridi majumbani na hivyo kuwezesha chakula kuiva kwa haraka.

Kwa mujibu wa Sescom, jiko la hilo limeundwa na sufuria maalum, vitambuzi vya halijoto na shinikizo, na kitufe cha kupunguza na kuongeza kasi ya umeme. 

Muundo wa jiko hilo humuwezesha mmiliki kutumia umeme mchache tofauti na anayetumia jiko la kawaida la umeme kupikia. 

Kwa nini jiko hilo?

Mkururugenzi Mtendaji wa wa Tatedo,  Estomih Sawe amesema majiko hayo yanaweza kuwa mbadala wa matumizi makubwa ya kuni na mkaa nchini. 

“Tani milioni moja inatumika hapa Dar es Salaam na hapa Dar es Salaam ni eneo ambalo karibu watu wote wana umeme, gesi na nishati zingine zote lakini bado wanatumia mkaa kwa wingi hivyo sisi tuliona umuhimu wa kuwa na teknolojia ya jiko linalotumia nishati kidogo sana ya umeme kuliko kutumia gesi, mkaa katika matumizi ya kupikia kwa haraka,” amesema Sawe.

Amesema kuna haja ya kuwahamasisha wananchi na kuwaelimisha ili wafahamu kuwa kuna nishati safi ambazo unaweza kutumia badala ya mkaa na ukapika chakula kwa bei nafuu, haraka na kwa usalama.

“Tunataka kuwakikishia kuwa lazima tuhamie teknolojia nyingine ya kupikia joto badala ya moto na natoa wito kwa Serikali na wananchi tushirikiane kuhusu kujua umuhimu wa kuwa na nishati mbadala katika kupikia na  upo uwezekano wa kupika kwa kutumia joto badala ya moto kwa ufanisi mkubwa na usiharibu mazingira,” amesema Sawe wakati akiongea na JikoPoint (www.jikopoint.co.tz). 

Ikiwa Watanzania watajikita katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ikiwemo majiko ya umeme wanaweza kuokoa miti mingi inayokatwa kila mwaka. Picha| Tatedo.

Faida za jiko la Sescom

Ukiwa utaamua kuanza kutumia jiko hilo ambalo kwa mujibu wa Sescom unatakiwa ujipange kidogo maana utalipata kwa Sh180,000. Hata hivyo, unaweza kulipia kidogo kidogo kulingana na uwezo wako. 

Jiko hilo lina uwezo wa kupika vyakula vya aina zote ikiwemo maharage, kande na nyama ambavyo huchukua muda mrefu kuiva. 

Meneja Nishati kutoka Tatedo, Mary Swai amesema wao waliamua kubuni jiko hilo la kisasa linaloweza kupika chakula chochote kwa gharama nafuu ili kuwapunguzia ukali wa maisha Watanzania. 

“Hili jiko yaani Pressure cooker ni jiko, sufuria na ni nishati ya kutumika nyumbani isiyo na moshi wala kuharibu mazingira unatumia umeme kidogo kuliko ungetumia mkaa na gesi,” amesema Swai na kusisitiza kuwa,

“Mfano umeweka dakika 30 ili kuivisha maharagwe au nyama au chakula kingine, pindi dakika hizo ulizoweka zikifikia basi jiko hujizima lenyewe lakini kikubwa katika jiko hilo ni kwamba linatumia sana joto katika kuivisha vyakula  badala ya moto.:

Lina uwezo wa kutumia uniti 0.2 hadi 0.3 za umeme kupika maharage. Pia linadumu kwa muda mrefu na haliunguzi chakula, hivyo halihitaji uangalizi wa karibu. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa