Kutana na majiko banifu yanayotumia umeme

Na Mariam John
31 Aug 2022
Majiko hayo yameundwa kutumia umeme kidogo hivyo kusaidia kutunza mazingira na afya za watumiaji.
article
  • Yanatumia kiasi kidogo cha umeme
  • Ni rafiki wa mazingira na afya za watu.
  • Yana uwezo wa kupika vyakula vya aina mbalimbali.

Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaomini kupikia chakula kwenye majiko ya umeme ni gharama, fahamu kuwa unahitaji elimu zaidi.

Nishati hiyo umeme ni rahisi na ya haraka kupikia, rafiki wa mazingira na afya ya mtumiaji. 

Majiko hayo hayatumii umeme mwingi tofauti na fikra za baadhi ya watu. Umeme kutumika mwingi inategemea na chakula unachopika au muda unaotumia jikoni.

Baadhi ya wabunifu wamebuni majiko banifu yanayotumia kiasi kidogo cha umeme, wakati huo kukidhi mahitaji ya mtumiaji. Baadhi ya majiko hayo ni yale yanayosambazwa na kampuni ya Jiko Chanya Ltd iliyopo mkoani Mwanza.

Kwa mjibu wa wakala wa majiko hayo, Doricus Nikolaus, majiko hayo hayatengenezwi nchini isipokuwa wanaagiza nje ya nchi.

Ametaja moja ya sifa ya jiko hilo kuwa halitumii umeme mwingi na unaweza kutumia umeme wa uniti 0.5 hadi 1 unaweza kupikia kwa saa moja kwa sababu “ jiko hili ni amara na salama.”

“Ni salama kwasababu hata mtoto anaweza kulitumia kwa sababu kama hujabandika sufuria jikoni jiko hilo litaendelea kuwa la baridi kabisa, joto litashika pale tu utakapobandika sufuria ya kupikia na baada ya kumaliza kupika linarudi kwenye ubaridi kawaida,” amesema Doricus.

Jiko hilo kwa kutumia sufuria maalum unaweza kuchoma nyama, kukaa chipsi bila kuweka mafuta na vyakula vingine vyote ambavyo unaweza kupikia kwenye nishati nyingine.

“Kwa kutumia jiko hili tunaweza kusababisha kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kutunza mazingira,” anasema Doricus.

Doricus yupo kwenye maonyesho ya wafanyabiashara ya Afrika Mashariki yanayoandaliwa Chemba ya Wafanya Biashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) ambayo hufanyika kila mwaka jijini Mwanza.

“Majiko haya yanaweza kutumia umeme kidogo mfano umeme wa Sh500 unaweza ukautumia kwa muda wa saa moja na nusu na kufanikiwa kuchemsha maharagwe ambayo ungetumia nishati nyingine ama majiko ya kawaida usingetosha” anasema Doricus mwenye uzoefu wa miaka miwili katika kazi ya kuuza majiko banifu.

Mwitiko wa ununuaji wa majiko hayo ni mkubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza huku akiwashauri baadhi ya Watanzania kuyachangamkia ili kuwa sehemu ya kutunza mazingira.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa