Kutana na mwanamke anayepambania matumizi ya gesi majumbani

Na Mariam John
8 Jul 2022
Joyce Mushi wa jijini Mwanza anatumia biashara yake ya gesi ya majumbani kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
article
  • Ni Joyce Mushi wa jijini Mwanza.
  • Anatumia biashara yake kutoa elimu ya matumizi ya gesi ya majumbani.
  • Lengo ni kuwakinga wanawake na athari za kiafya za kuni na mkaa.

Ni saa tano asubuhi katika Mtaa wa Usagara jijini Mwanza. Hapa ndipo utamkuta mama huyu akiendelea na shughuli yake ya kuuza bidhaa za nyumbani katika duka lake.

Licha ya kuuza bidhaa za nyumbani, nje ya duka lake amepanga mitungi ya gesi ya majumbani (LPG) ambayo huwauzia wateja wanaokuja katika duka lake. 

Joyce Mushi, mkazi wa Halmashauri ya Nyamagana jijini hapa ni miongoni mwa wanawake nchini Tanzania ambao wako mstari wa mbele kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ili kuokoa mazingira. 

Joyce anasema gesi anayouza siyo tu inamuingizia kipato cha kuendesha familia bali inasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa. 

Ni zaidi ya kuuza gesi na mitungi yake

“Nimeanza kazi ya uwakala wa kuuza mitungi ya gesi miaka mitatu iliyopita wakati huo matumizi ya gesi yalikuwa chini sana, ni wachache ambao walinunua au kubadilisha, wengi waliogopa kuwa huenda inaweza kulipuka isipofungwa vizuri,” anasema Joyce.

Mama huyo wa watoto watatu anasema haikua rahisi watu katika eneo lake kukubali kutumia gesi kupikia chakula nyumbani kutokana mazoea waliyokuwa nayo ya kuni na mkaa.

Hata hivyo, hiyo ilikuwa fursa ya kupata soko na kuongeza matumizi ya nishati hiyo katika kaya. 

Wakati wa kuuza na kusambaza gesi hizo kwa wateja wake, amekuwa akitoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na salama ya kupikia hasa gesi ya majumbani.

Anasema anatoa elimu hiyo kwa sababu yeye ni muathirika wa kiafya wa matumizi ya kuni na mkaa ambapo awali alikuwa akipata matatizo ya kupumua na macho.

Sasa matatizo hayo hayapati tena kwa sababu amehamia katika matumizi ya gesi ya kupikia chakula nyumbani.

Gesi ya mtungi wa kilo sita huuza kwa Sh24,000 huku wa kilo 15 huuza kwa Sh59,000 hadi Sh60,000. Hata hivyo, bei hutegemea kampuni ya gesi inayosambaza mitungi hiyo.

Gesi ya majumbani inarahisisha upikaji wa chakula kwa sababu hutumii nguvu na muda mwingi kuipata na kuitumia. Picha| EATV.

Kupitia elimu ya matumizi ya gesi anayotoa imechangia kuongeza idadi ya wateja kwenda kununua gesi katika duka lake ambapo kwa siku hakosi angalau watu watano wanaokwenda kupata huduma hiyo.

“Zamani matumizi ya gesi yalikuwa chini kwa kuwa watu walikuwa na hofu ya kutumia na wengine hawakujua kabisa namna ya kutumia. Ilinilazimu kuingia gharama ya muda kuwaelesha watu namna ya kutumia mtungi na jiko hilo la gesi, elimu ambayo najivunia imekuwa na mapinduzi makubwa kwa wananchi,” anasema Joyce.

Licha ya kuwa bado hajawafikia watu wengi, elimu hiyo pia imesaidia kuondoa dhana potofu kuwa gesi inapika chakula laini peke yake, jambo ambalo siyo kweli kwa sababu nishati hiyo ni suluhisho la vyakula vyote.

Katika madarasa yake amekuwa akifundisha urahisi anaopata mtu akiwa ataamua kutumia gesi. Kwanza anapunguza muda anaotumia jikoni na anaweza kupika vyakula vingi kwa wakati mmoja kwa muda mfupi.

“Kwa hiyo mtu anachagua atumie tu gesi ili kurahisisha katika kupika, anatumia muda mchache kwenye kupika chakula hata kama ni kigumu kuliko kwenye mkaa ambapo itakulazimu utumie muda mrefu zaidi,” anasema mama huyo.

Biashara ya gesi yamtoa kimaisha

Uuzaji wa gesi umemsaidia Joyce kupata kipato cha ziada, tofauti na zamani ambapo alikuwa akitegemea duka la bidhaa za nyumbani pekee. 

Biashara hiyo inamsaidia kupata kipato kukidhi mahitaji ya familia na kusomesha watoto wake ambapo mmoja yuko chuo kikuu. 

Maono yake ni kuona wanawake wenzake wanageukia matumizi ya gesi na kuachana na mkaa na kuni ili kufaidika kiuchumi na kiafya.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa