Kwa nini wanawake wawekeze katika nishati safi na salama?

Na jikopoint
11 Aug 2022
Nishati hizo ikiwemo majiko ya gesi ya majumbani yatawasaidia kulinda mazingira, kuboresha afya na kupata kipato kuendesha maisha..
article
  • Itawasaidia kupata fedha kuboresha maisha yao na kupunguza utegemezi.
  • Pia ni fursa kushiriki katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Biashara ya gesi ni nzuri ukiuza mtungi hapo hapo unatenga faida yako hii ni biashara inayoeleweka,” anaeleza Neema Mwakagila, mfanyabiashara wa gesi ya majumbani (LPG) mkoani Mbeya.

Neema anayefanyia shughuli zake Mtaa wa Mkombozi, Kata ya Luanda mkoani hapa anasema hiyo ni fursa ya kujiajiri kwa mabinti katika sekta ya nishati safi na salama. 

Licha ya kuwa ni fursa ya kuboresha maisha na mazingira, kasi ya elimu kuhusu nishati hiyo ikiwa ndogo huenda ikachukua muda mrefu kwa wanawake kufaidika nayo.

Neema ambaye ni bachela ameamua kuwa mtoa elimu muuzaji wa gesi hiyo kwa wanawake wenzake ili kuwapunguzia mzigo wa kutumia kuni na mkaa ambao umekuwa na athari mbalimbali za muda mfupi na muda mrefu. 

“Mtu akinunua mtungi wa gesi  lazima umuelekeze mteja namna ya kutumia gesi cha kuzingatia ni ile burner (kifungio)  lazima ufunge kwa usahihi  watoto  wasichezee, lakini gesi haina madhara kama watu wanavyosema,” anaeleza binti huyo.

Ikiwa kila muuzaji na msambazaji wa gesi ya majumbani akatumia vizuri biashara yake kutoa elimu kwa watu anaowahudumia itasaidia kuongeza kasi ya matumizi ya nishati hiyo kwa wanawake katika kupikia nyumbani na kwenye biashara.

Uanzie wapi kufanya biashara ya gesi?

Neema mwenye uzoefu wa zaidi ya mwaka mmoja katika biashara hiyo, anasema wanawake wanaweza kuanza kuuza gesi katika maeneo yao kwa mtaji mdogo na kuwashawishi watu waache mkaa na kuni na waanze kutumia nishati hiyo.

Kwa mujibu wa binti huyo, biashara hiyo inahitaji muuzaji mwenye uwezo kuelewa mtazamo na uelewa wa watu kuhusu nishati ya kupikia ambapo watu wakielewa faida za gesi ya majumbani ni rahisi kuachana na nishati chafu. 

“Nawashauri wafanye hii biashara unaweza ukaanza na mtaji mdogo unakuwa unaendelea kadiri siku zinavyoenda unapata faida yako na unaongeza mtaji,” anasema.

“Kwa mfano mimi ni msichana mdogo wala sijaolewa na sina sapoti kwa hiyo unaweza kufanya biashara na kuweka vipaumbele vyako.”

Kwa siku, binti huyo huuza mitungi ya gesi mitatu hadi mitano yenye kilo 6 na kilo 15 na hivyo kujipatia kipato japo kidogo kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Matarajio yake ni kukuza biashara hiyo na kuw amsambazaji mkubwa gesi hiyo kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila siku kutokana na viongozi wa dunia kuongeza msukumo katika kukabiliana na athari za ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni.

Anasema hali ya soko la gesi iko vizuri lakini changamoto kubwa ni bei. Mabadiliko ya bei yanasababisha kukosa wateja kwa sababu kwa sasa mtungi mdogo wa kilo 6 unauzwa kwa Sh25,000 kutoka Sh22,000 bei ya zamani.

Kwanini gesi ya majumbani?

“Gesi ina mchango mkubwa sana katika utunzaji wa mazingira kwa sababu, kuni na mkaa inachafua mazingira, gesi unatumia kwenye nyumba yoyote na katika mazingira yoyote,” anasema Neema ambayo ni mtumiaji mzuri wa nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, asilimia 89 ya kaya za Tanzania hutumia kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Jambo hili husababisha uharibifu wa mazingira na afya za watu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa