Mabadiliko ya tabianchi: Fursa kwa wanawake kutumia gesi ya majumbani

Na jikopoint
10 Aug 2022
Gesi ya majumbani inaokoa muda, inasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa na hivyo kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi.
article
  • Wahimizwa kutumia nishati hiyo kukabiliana na ukame.
  • Pia itawasaidia kupata kipato na kupunguza gharama manunuzi ya nishati.

Wakati Watanzania wakiendelea kutegemea mkaa na kuni kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia, baadhi ya wanawake nchini Tanzania wamebadilisha mtazamo na kuanza kutumia kikamilifu fursa za nishati safi na salama kujiingizia kipato na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Angel Msigwa, mkazi wa Njombe mjini ni miongoni mwa wanawake ambao wameachana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni na kujikita katika matumizi ya gesi ya majumbani (LPG)

Angel maarufu kama mama Dani, licha ya kuwa anatumia gesi kupikia lakini ameamua kujiajiri katika biashara ya kuuza gesi hiyo ili kujiingizia kipato kwa ajili ya kusongesha maisha na familia yake.

“Mimi natumia gesi nyumbani kwangu, kwa sasa mkaa situmii kabisa,” anasema Mama Dani akiwa katika duka lake analouza mitungi ya gesi ya majumbani mjini Njombe.

Mama huyo ambaye ameajiri wafanyakazi wawili katika duka lake kumsaidia kusambaza gesi, amekuwa balozi wa gesi ya majumbani. Anaitumia biashara yake kuwahimiza wanawake kutumia nishati hiyo ili kulinda afya zao na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Nimekuwa nikitoa elimu kwa watu hasa wanawake watumie gesi nyumbani, ina faida nyingi kwa mazingira na afya,” anasema Mama Dani.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, asilimia 89 ya kaya za Tanzania hutumia kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Jambo hili husababisha uharibifu wa mazingira na afya za watu.

Kwanini gesi na siyo mkaa au kuni

Mama Dani mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka miwili ya uuzaji wa gesi anasema athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, kubadilika badilika kwa unyeshaji wa mvua kunakosababishwa na ukataji wa miti, ndiyo kulimfanya aanze biashara hiyo.

“Unaona sasa hivi hata hali ya hewa yenyewe Njombe imebadilika, tumekata sana miti, maji yenyewe tulikuwa hatusumbuki miaka ya nyuma, lakini sasa hivi mkaa umeleta shida,” anasema, “wamekata miti hadi sehemu ya vyanzo vya maji.”

Licha ya kuuza bidhaa hiyo lakini anatoa elimu kwa majirani na watu wanaomzunguka kutumia gesi ya majumbani ili kupunguza ukataji wa miti na kuokoa mazingira. 

“Ambao hawawezi kutumia gesi pia tunawashawishi watumie mkaa mbadala ili tutunze mazingira,” anasema Mama Dani ambaye anaamini kuwa kila mtu akiwajibika na kugeukia nishati safi na salama, basi dunia itakuwa sehemu salama ya kuishi.

Akielezea zaidi kuhusu matumizi ya gesi ya majumbani kwa ajili ya kupikia nyumbani na kwenye biashara, anasema gesi inaokoa muda wa kupika chakula kwa sababu inapatikana kirahisi hasa katika maeneo yenye mfumo mzuri wa usambazaji. 

“Nilijaribu kuangalia kwenye jamii yangu watu ninaowazunguka na wanaonizunguka, nikaona watu wapo bize na maisha. Kwa hiyo unakuta mtu kuanza atafute mkaa, akoleze, atafute vikuni na makaratasi ndiyo aanze kuwasha moto anapoteza muda,” anasema Angel.

Tatizo hilo la kutumia muda mwingi katika kuandaa mkaa jikoni akaligeuza kuwa fursa ya kuanza kuwashawishi na kuwauzia gesi majirani zake ili mkono uende kinywani.

Gesi anayouza Angel ni ile inayohifadhiwa katika mitungi midogo ya kilo 6 na kilo 15 ambayo hutumiwa zaidi majumbani.

Nishati hiyo safi ya kupikia pia hupunguza athari za muda mrefu za kiafya ikiwemo matatizo ya macho na mfumo wa hewa ambayo ni vigumu kugundua.

“Kuna watu unakuta wanasumbuliwa na macho. Hao wenye shida ya macho ukija kufuatilia chanzo ni nini? unakuta alikua anatumia mkaa na kuni,” anasisitiza.

Angel Msigwa (kulia) akimuonyesha mteja aliyekuja kununua gesi dukani. Gesi ya majumbani inasaidia kupunguza ukataji wa miti. Picha| Imani Henrick.

Changamoto kibiashara

Kupanda kwa bei ya gesi wakati mwingine kumekuwa kukiwakimbiza wateja wa Angel na baadhi yao kulazimika kurudi katika matumizi ya mkaa au kuni. 

Angel ameiomba Serikali na wadau wa nishati ya gesi kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku katika nishati hiyo ili kuvutia watu wengi zaidi kuitumia, jambo likalosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa sasa, katika maeneo mbalimbali ya Njombe Mjini gesi ya majumbani inauzwa Sh25,000 kwa mtungi wa kilo 6 huku ule wa kilo 15 unauzwa kati ya Sh59,000 hadi Sh60,000. 

Anasema mchakato wa kubadilisha fikra za watu kuhamia katika matumizi ya gesi huchukua muda mrefu kutokana na mazoea waliyonayo juu ya mkaa na kuni, hivyo uvumilivu unahitajika katika kuwaelekeza. 

Serikali mstari wa mbele nishati safi

Waziri wa Nishati, January Makamba katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka mwaka 2022/23 alisema Serikali imetenga Sh500 milioni ili kufanya kampeni kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora ya kupikia pamoja na tafiti za kubaini nishati, mfumo sahihi na vivutio vya kusambaza nishati hiyo kwa maeneo ya vijijini.

“Vilevile katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imepanga kutumia Sh10 bilioni  kutekeleza mradi wa kupeleka na kusambaza gesi asilia katika makazi ya wananchi walio katika mkuza wa bomba kuu la gesi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani,” alisema Makamba.

Mradi huu kwa maeneo ya vijijini ambao ni wa kwanza hapa nchini utakuwa wa majaribio. Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)  itaendelea kutoa ruzuku kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na wadau wengine ili kupanua huduma hizo katika maeneo mengi zaidi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa