Mambo ya kuzingatia katika kufanya biashara ya nyama choma

Na Lucy Samson
22 Jul 2023
Kabla ya kuanza shughuli ya kuchoma nyama ni vyema uzingatie suala la kujisajili ili utambulike na upewe kibali cha kufanya shughuli hiyo.
article
  • Ni pamoja na usajili, usalama wa eneo la kuchomea nyama.
  • Elimu na afya ya mchomaji ni jambo la kuzingatia pia.

Biashara ya nyama choma ni moja ya shughuli maarufu katika maneno mengi nchini ikiwaingizia kipato watu wengi wanaojishughulisha nayo.

Miongoni mwa nyama maarufu zinazotumika katika biashara ya nyama choma ni Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Nguruwe na kuku. Nyama hizo hutumika kuandaa aina mbalimbali za mapishi ya nyama choma kama mapande, mishikaki, na “foil”. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi uzalishaji wa nyama nchini umeongezeka kwa asilimia 4.3 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mwaka 2022/2023 tani 803,264 za nyama zilizalishwa ulinganisha na 

tani 769,966 zilzozalishwa mwaka 2021/2022, jambo linalochangia kuimarika kwa biashara za nyama ikiwemo uchomaji na kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi nchini.

Ikiwa una malengo ya kutoa huduma ya nyama choma siku za mbeleni, Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imeanisha mambo muhimu ya kuzingatia katika ufanyaji wa biashara hiyo yatakayohakikisha usalama wa wateja wako na uhalali kibiashara.

1.Usipende kona kona, jisajili 

Kabla ya kuanza shughuli ya kuchoma nyama ni vyema uzingatie suala la kujisajili ili utambulike na upewe kibali cha kufanya shughuli hiyo.

TMB inasema usajili huo unafanyika kupitia mfumo wa Usajili wa Vibali MIMIS unaofanyika mtandaoni kupitia tovuti yao. Usajili katika mamlaka husika unaweza kukusaidia kupata dili kubwa kubwa za kampuni na mashirika nyakati za sherehe. 

Aina hizi za kandarasi mara nyingi huwa na malipo mazuri ukilinganisha na mtu mmoja mmoja na ni njia nzuri ya kukuza biashara yako kwa haraka. 

2.Hakikisha eneo la kuchomea nyama linafikika kirahisi

Bodi ya nyama inashauri kuwa eneo linalotumika kuchomea nyama ni lazima liwe rahisi kufikika na lisiwe kwenye mazingira ambayo ni rahisi kupata mafuriko, kutuama maji machafu au vumbi. 

“Mazingira ya kuchomea nyama yawe mbali anagalau mita 100 na sehemu zinazozalisha uchafu kama mitaro ya maji taka, mashimo na maeneo ya kunyolea au kusukia,” imesema bodi katika moja ya vipeperushi vyake vinavyotoa elimu ya uchomaji nyama.  

3.Hakikisha nyama yako imepimwa na wataalamu

Nyama ya kuchomwa ni lazima itolewe kwenye machinjio au maeneo yaliyoidhinishwa kuchinja wanyama yaliyoidhinishwa na bodi ya nyama.

Mfanyabiashara ni lazima uhakikishe nyama unayonunua imekaguliwa na kugongwa muhuri. Hii itasaidia kuongeza imani ya wateja wako kuwa unauza chakula kilicho halali na si vinginevyo. Ni hatari kibiashara siku igundulike unauza nyama kutoka machinjio bubu ambayo nyama zao hazipimwi. 

Bodi inashauri pia nyama ibebwe na kusafirishwa katika magari maalumu ya kuhifadhia nyama ilikuepuka vimelea vya magonjwa na kuharibika.

 4.Hifadhi nyama mahali salama

Tumezoea kuona nyama ikifadhiwa katika majokofu au sehemu za baridi kuzuia zisiharibike. Hata hivyo, bodi ya nyama inasisitiza kuwa jokofu hilo ni lazima liwe safi na isichanganywe na bidhaa nyingine.

Pamoja na hayo, chumba kinachotumika kuhifadhi nyama lazima kiwe na hewa safi na uwezo wa kudhibiti viumbe waharibifu kama panya ambao pia husambaza magonjwa. 

Kumbuka mtu akipata madhara ya kiafya kama kuhara na mengineyo baada ya kula nyama choma yako si rahisi kurejea tena au kuwashauri wengine waje kununua kwako.

Ni vyema kuhakikisha mikono yako ni misafi wakati wowote unapochoma nyama.Picha|Rud’s Farm/Instagram.

5.Ubora wa jiko la kuchomea

Kama jiko lako lina kutu, limechakaa au lina vumbi bodi ya nyama inasema jiko hilo halifai katika shughuli ya kuchomea nyama.

Ili nyama unayochoma iwe salama hakikisha jiko unalotumia ni la kufunika, halina kutu, sumu wala viambata sumu. Hii itasaidia kuhakikisha usalama wa nyama na afya wauzaji na watumiaji wa huduma yako. 

Baadhi ya wateja hufanya uamuzi wa kununua nyama kwa kuangalia tu mazingira inapoandaliwa likiwemo jiko. Wengine wanaweza kususa kununua nyama yako kwa sababu ya uchafu wa jiko lako. Upo tayari kupoteza wateja na faida kwa sababu ya jiko? 

6.Elimu na kiwango cha ujuzi wa kuchoma nyama

Si kila mtu anaweza kujiingiza katika shughuli hii bila kupata elimu stahiki zinazotambulika.

TMB inasema mchoma nyama anagalau awe na cheti cha msingi cha uchomaji wa nyama au kupata mafunzo ya utendaji wa kazi kwa kuzingatia usalama na ubora (GHP). Baadhi ya mafunzo hayo yanapatikana katika vyuo vya ufundi stadi kama Veta au vyuo vinavyotoa mafunzo ya upishi. 

7.Zingatia afya

Ikiwa unafanya biashara hii ya kuchoma nyama hakikisha unapima afya kila baada ya miezi mitatu na uvae sare maalumu kama aproni, kofia na buuti nyeupe wakati wote unapofanya shughuli hizo pia zingatia usafi wa nywele na kucha. 

Haipendezi mchoma nyama kuwa rafu, kucha ndefu na mwenye nguo chafu kiasi cha kutia kinyaa wateja. 
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) linasema ili kudumisha usafi ni vyema kuosha mikono katika mabomba yanayotakiwa kuwepo katika sehemu za kuandaa nyama.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa