Mkaa mbadala unavyoinua maisha ya mama lishe Tanzania

Na Esau Ng'umbi
28 Jul 2022
Umewasaidia wanawake wanaouza chakula kupunguza gharama za kununua mkaa na hivyo kuongeza faida katika biashara zao jijini Dar es Salaam.
article
  • Ni kupitia faida wanayoipata kwa kutumia mkaa mbadala kwenye shughuli zao.
  • Unatengenezwa kwa taka za majumbani ikiwemo vifuu vya nazi, maganda ya ndizi na mihogo.
  • Waomba Serikali kuviwezesha vikundi vinavyotengeneza mkaa huo ili upatikane kwa wingi.

Dar es salaam. Katika moja ya kibanda kilichopo Mtaa wa Msimbazi, Tabata jijini Dar es salaam, mama huyu anaendelea kuwahudumia chakula wateja wake ambao wanaingia na kutoka.

Ni Warda Omary, mama lishe anayefanya shughuli zake za kupika chakula karibu na soko la Tabata Muslim, Halmashauri ya Wilaya ya Ilala.

Kwa siku moja huingiza wastani wa Sh40,000 hadi Sh50,000 katika biashara hiyo na faida anayoipata baada ya kutoa gharama za uendeshaji ni Sh10,000 au zaidi.

Hata hivyo, Warda (44) angetumia muda mrefu kuipata faida hiyo kama asingeanza kutumia mkaa mbadala kwenye shughuli yake ya mama lishe. miaka mitatu iliyopita.

Warda ambaye alianza kutumia mkaa mbadala miaka mitatu iliyopita hana bajeti ya kununua nishati hiyo kwa sababu ana ujuzi wa kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia taka kama vile vifuu vya nazi, maganda ya ndizi pamoja na maganda ya muhogo, 

Kupitia mkaa mbadala ameweza kuokoa wastani wa Sh5,000 kila siku ambayo angeitumia kununua mkaa wa kawaida kukamilisha mapishi katika mgahawa wake.

“Mkaa mbadala una mchango mkubwa sana kwenye biashara yangu, kabla sijaanza kutumia mkaa mbadala nilikuwa napata faida kidogo, nilikua natumia mkaa wa Sh3,000 hadi Sh5,000 kwa siku.

“Kama ningekuwa nanunua mkaa mbadala ningekuwa natumia Sh2,000 lakini siingii gharama kwa kuwa nautengeneza mwenyewe hivyo napata  faida,” anaeleza Warda. 

Warda Omari akiendelea na shughuli ya kupika katika kibanda chake kilichopo Mtaa wa Tabata Msimbazi jijini Dar es Salaam. Anapika kwa kutumia mkaa mbadala. Picha| Daudi Mbapani.

Safari ya kujikwamua kiuchumi

Warda ana uzoefu wa miaka 12 katika shughuli ya mama lishe lakini alianza kutumia mkaa mbadala mwaka 2019 baada kupata  mafunzo ya kutengeneza mkaa huo kutoka kwa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Forum on Climate Change (ForumCC) inayojihusisha na utoaji wa elimu ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Nilipopata mafunzo nilianza kujifunza kutengeneza mimi mwenyewe na baadaye kuanza kuutumia kwenye biashara yangu,” anasema Warda mwenye familia ya watoto wanne.

Awali alianza kutengeneza mkaa wa makaratasi pekee ambapo alikuwa anayakata katika vipande vidogo vidogo kisha kuyaloweka kwenye maji. Baada ya makaratasi kuloa, huyatoa kwenye maji na kuunda vidonge vidogo na kuanika juani kabla ya kutumia.

“…tulipopata mafunzo zaidi tukaanza kutengeneza mkaa mzito kwa kutumia vifuu, maganda ya ndizi na maganda ya mihogo,” anasema Warda.

Majirani wanasemaje?

Si Warda pekee mwenye ushuhuda juu ya faida za mkaa mbadala kwenye shughuli za mama lishe. 

Ashura Hussein Maige maarufu kama mama James anaihudumia familia yake kupitia biashara hiyo ya chakula anasema mkaa huo umempunguzia gharama za maisha tofauti na alipokuwa akitumia mkaa wa kawaida.


“Mkaa mbadala ni mzito tofauti na mkaa wa kupima, nikichukua mkaa wa Sh5,000 huwa napikia siku nne, wakati huu wa kawaida kwa siku natumia mkaa wa Sh7,000 kwa hiyo kwa upande wangu nauona mzuri,” anasema mama James ambaye amekuwa akifanya biashara hiyo kwa miaka mitano sasa katika soko la Tabata Muslim. 

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Fahari Yetu wakiendelea na shughuli ya kutengeneza mkaa mbadala kwenye kiwanda chao kidogo kilichopo Tabata, Dar es Salaam. Picha| Daudi Mbapani.

Kibarua walichonacho

Pamoja na mkaa mbadala kuwafaidisha akina mama lishe hawa, bado upatikanaji wa nishati hiyo inayopigiwa chapuo katika utunzaji wa mazingira siyo wa kuridhisha kutokana na teknolojia duni ya utengenezaji wa mkaa huo, jambo linalosababisha wakati mwingine kurudi katika matumizi ya mkaa wa kawaida.

Ashura anasema kama watengenezaji wa mkaa huo  wakishikwa mkono na Serikali au na taasisi yoyote kwa kuwanunulia mashine itakayoongeza uzalishaji na kuwahakikishia upatikanaji wa bidhaa hiyo na wao wataongeza kipato. 

“Tatizo kubwa kwenye huu mkaa mbadala yani uzalishaji umekuwa mdogo kwa hiyo tumekuwa tunautumia kwa muda ambao wanautengeneza baadaye unakuwa hamna tunarudi tena kwenye wa kawaida,” anasema mama James.

Warda ambaye amejenga nyumba yake kwa biashara ya mgahawa amewashauri wanawake wengine wanaofanya biashara ya chakula kugeukia mkaa mbadala ili kupunguza gharama za maisha. 

“Napenda kuwaambia akina mama wengine wanaofanya biashara kama yangu na wanaokaa majumbani nawashauri watumie mkaa mbadala ni rahisi na unaokoa bajeti,” anasema Warda.

Mkaa huo licha ya kukaa muda mrefu kwenye jiko, bali unasaidia kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Pia unapunguza uchafu kwenye mitaa na sokoni. 

Unaweza kuwasiliana na mwalimu wa mkaa mbadala Warda Omary kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia

namba 0712 343601.

.JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa