Muuza majiko banifu mwenye ndoto ya kuwaondolea umaskini wanawake

Na Lucy Samson
9 Jul 2022
Ni Jackline Julius anayeuza na kutoa elimu ya matumizi ya majiko banifu yanayotumia yanayotumia gesi, mkaa na kuni chache.
article
  • Ni Jackline Julius anayeuza majiko yanayotumia yanayotumia gesi, mkaa na kuni chache.
  • Yanasaidia kupunguza ukataji miti na kuokoa afya za wanawake.
  • Ana ndoto za kumfikia kila mwanamke kwa nishati safi na salama.

Katikati ya kundi la kundi la watu 10, amesimama binti huyo aliyevalia kofia nyeusi, shati ya kijivu na suruali ya bluu akiwaeleza kwa ujasiri na tabasamu watu waliomzunguka.

Hapa ni katika banda mojawapo lililopo katika viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam. 

Ni Jackline Julius, Meneja Masoko wa majiko banifu wa kampuni ya Jikokoa akiwaelewa watu hao waliotembelea  banda lake namna majiko hayo yanavyofanya kazi. 

Jikokoa linalotumia nishati ya mkaa na kuni kwa kiwango kidogo ukilinganisha na majiko mengine.  Limebuniwa na na kutengenezwa na  kampuni ya Burn ya nchini Kenya. Kwa Tanzania bidhaa hiyo inapatikana Goba jijini Dar es Salaam.

Licha ya Jackline (28) kuwa katika kampuni hiyo kama mfanyakazi lakini ni miongoni mwa wanawake ambao wanatumia vizuri fursa ya kuajiriwa kuchagiza matumizi ya teknolojia rahisi zinazopunguza uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti. 

Kazi anayofanya binti huyo ina mchango mkubwa katika safari ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ili kuboresha maisha, kuokoa mazingira na kutengeneza ajira hasa kwa wanawake ambao ni waathirika wa matumizi ya kuni na mkaa.

Muundo wa jiko hilo banifu

Jiko hilo lenye umbo la duara limetengenezwa kwa mabati na vyuma ambapo lina sehemu ya kuwekea kuni, mkaa na sehemu ya kuliunganisha na mtungi wa gesi ya majumbani (LPG). 

“Hili jiko unapikia sehemu yoyote unaweza kulitumia kama gesi unaliweka hata ndani, ni rafiki wa mazingira kwa kweli,” anasema Jackline.

Muundo wake umebuniwa kutumia mkaa na kuni kidogo. 

Jiko dogo linauzwa Sh120,000, saizi ya kati linalouzwa Sh130,000 na jiko kubwa (pro) linauzwa kwa Sh220,000. Pia kuna jiko linalotumia kuni tu ambalo linauzwa Sh110,000.

Majiko haya yametengenezwa maalumu kwa mapishi ya nyumbani na wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo mama lishe wanaotumia nishati ya mkaa au kuni.

Jackline Julius akitoa maelezo ya jinsi ya kutumia jiko banifu katika maonyeshi ya kimataifa ya biashara ya Sabasaba kwa mwaka 2022. Picha | Daudi Mbapani.

Mwanafunzi, mwalimu mhamasishaji

Jackline anayeishi Segerea jijini hapa anasema alianza kutumia majiko hayo mwaka 2021 kabla ya kuanza kuyauza na kuyasambaza katika sehemu mbalimbali jijini hapa.

“Nilivutiwa na teknolojia hii, yani hainiathiri chochote zaidi inanisaidia kupika kwa haraka,” anasema Jackline na kubainisha kuwa hakupenda kuona manufaa hayo yanamnufaisha peke yake.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kueneza elimu hiyo kwa watu mbalimbali kupitia kazi yake ya meneja masoko ambayo inampa fursa ya kukutana na watu.  

Anasema wakati akipato kipato katika kazi hiyo, wakati huo huo anatoa mchango wake katika utunzaji wa mazingira kwa kuwahimiza watu kutumia majiko hayo banifu. 

Akiendelea kutoa elimu kwa wateja wanaoingia na kutoka katika banda  hilo, anasema jiko hilo lina faida nyingi endapo mtu ataamua kulitumia. 

Linadumu muda mrefu

Jikokoa limetengenezwa kwa tecknolojia isiyoruhusu kupata kutu ili lidumu kwa muda mrefu ukilinganisha na majiko ya mkaa ya udongo yanayoharibika haraka.

Jackline ni shuhuda wa jinsi Jikokoa linavyoweza kudumu muda mrefu. Tangu anunue mwaka mmoja uliopita bado jiko lake lina muonekano mzuri. 

Ameweza kuokoa fedha ambazo angenunua majiko ya kawaida hadi sita kwa mwaka mmoja.

“Kwa majiko ya kawaida ningekuwa nimenunua majiko sita ndani ya mwaka mmoja unakuta lina haribika unanunua tena, wakati huo huo inakubidi ununue mkaa mwingi,” anasema binti huyo.

Majiko banifu yanayotumia mkaa na kuni chache pia gesi ya majumbani. Majiko hayo yanapunguza ukataji wa miti. Picha | Daudi Mbapani.

Mkaa mchache mapishi mengi

Jikokoa linatumia mkaa mchache hii ni kutokana na jinsi lilivyotengezwa. Nafasi ndogo kwa ndani pia muundo wake wa chuma unaruhusu kutunza joto hata wakati mkaa ukiwa umeisha.

Jackline anasema jiko hilo lina uwezo wa kutumia mkaa gunia moja tu kwa miezi mitatu, ukilinganisha na majiko mengine.

“Unajikuta kwa mwezi unatumia gunia moja la mkaa kwa miezi mitatu tofauti na jiko la udongo ambalo gunia moja halitoshi kwa mwezi (kwa familia yenye watu wengi),” anasema Jackline.

Kupunguza ukataji miti

Jikokoa ni rafiki wa mazingira kwa sababu limeundwa kupunguza ukataji wa miti katika nchi za Afrika, anasema binti huyo ambaye wakati wote sura yake imechangamka. 

Kwa mujibu wa kampuni ya Jikokoa, jiko hilo likitumika vizuri linaweza kuokoa mkaa kilo 204 kila mwaka na hivyo kupunguza kiwango cha ukataji miti.

Kwa mujibu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), inakadiriwa kwa mwaka heka zaidi ya 300,000 za miti hukatwa nchini kila mwaka kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa.

Kupunguza uchafuzi wa hewa

Majiko ya mkaa na kuni huzalishwa kwa wingi moshi ambao huchangia  uzalishaji wa gesijoto ambayo huwa na mchango mkubwa katika mabadiliko ya tabianchi.

“Majiko haya hayana moshi kabisa unaweza hata kupikia ukiwa ndani na mlango ukiwa umefungwa,” ameongeza Jackline.

Kwa sasa, Tanzania inachangia asilimia 0.36 ya gesijoto yote inayozalishwa duniani huku ikijiwekea malengo ya kupunguza uzalishaji huo kati ya asilimia 30 hadi 35 ifikapo mwaka 2030. 

Moja ya mikakati kufikia shabaha hiyo ni kuhimiza jamii kutumia nishati safi na salama kama inavyofanya Jikokoa.

Anavyowapata wateja wa majiko hayo 

Akiwa kama meneja masoko, maonyesho ya sabasaba ni fursa wanayoitumia kujipatia wateja ambapo wateja wanaopita kwenye banda lao hupata nafasi ya kununua bidhaa na kupewa mawasiliano atakayoyatumia wakati wowote atakapohitaji jiko. 

“Mteja yoyote atakayepita kwenye banda letu awe amenunua au hajanunua lazima tuchukue mawasiliano yake ili tuwasiliane nae akihitaji jiko,” anasema Jackline.

Njia nyingine ambayo hutumika baada ya maonyesho ni  matangazo kwa kutumia magari barabarani, ambapo wateja hupata nafasi ya kusikia  na kuona bidhaa na kuweza kununua.

Uuzaji wa majiko banifu umebadilisha maisha yake

Kazi hii imekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Jackline kumuwezesha kuendesha maisha yake, ambacho ni zaidi ya kile alichokipata kwenye kazi ya hoteli aliyokuwa akiifanya mwanzoni.

Mbali na kumuingizia kipato, kazi hiyo imefanya kujiwekea akiba, kwani yeye pia ni mtumiaji namba moja wa Jikokoa, ambayo anasema limempunguzia matumizi ya mkaa kwa kiasi kikubwa.

“Pesa iliyotakiwa kununua mkaa au kununua majiko mengine baada ya yale ya mwanzoni kuharibika naweza kupeleka watoto shule,au kuwanunulia madaftari,” anasema Jackline.

Jiko hilo banifu pia linapunguza gharama za maisha hasa bajeti ya nishati ya kupikia. Pia linamuepusha mtumiaji na athari za afya zinazotokana na moshi. Picha| Daudi Mbapani.

Ugumu wa kazi hiyo

Changamoto kubwa anayokumbana nayo binti huyo ni kumuelewesha mteja utofauti wa Jikokoa na majiko mengine ya udongo au mabati ambayo watu wengi wanadai wamezoea kuyatumia.

“Kuna wengine wanataka uwatofautishie kati ya hii na ile au bidhaa unayouza ina ubora gani,” anasema Jackline.

Mbali na changamoto hiyo, baadhi ya wateja hutaka kuletewa majiko majumbani lakini hawako tayari kulipia gharama za usafiri, “hivyo kama meneja masoko au kampuni kwa ujumla jambo hilo linatuumiza.”

Atoa somo kwa wanawake

Licha ya kufanya kazi ya kuuza majiko banifu hayo kwa kipindi cha miezi sita, anatamani bidhaa hiyo imfikie kila mwanamke nchini Tanzania kutokana na faida zake.

“Kwanza inaokoa fedha yako wewe mama hata baba akikuachia ununue mkaa wa Sh15,000 ukitumia Jikokoa unajikuta umenunua mkaa wa Sh4,000 hela nyingine unaweza kupeleka Vikoba” anasema.

Majiko hayo ni ajira kwa wanawake, Jackline anasema wanaweza kujiajiri kwa kuyauza na kutoa elimu kwa watu wanaoishi nao karibu. 

Kupata taarifa zaidi kuhusu majiko hayo, unaweza kumpata Jackline Julius kwa namba hii 0785123739.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa