Safari ya mwalimu wa mkaa mbadala Dar es Salaam – 2

Na Daniel Samson
26 Jul 2022
Tausi anasema licha ya kukubalika zaidi na wanawake wenzake, wako baadhi ya wanaume akisimama mbele kufundisha kuhusu mkaa mbadala humchukulia poa wakidhani hawezi kutoa maarifa yanayoweza kubadilisha maisha yao.
article
  • Ni Tausi Msangi mkazi wa Kipunguni Dar es Salaam.
  • Anaeneza elimu ya mkaa mbadala kila kona jijini.

Licha ya kuwa sasa ni moja ya walimu bora wa kutengeneza mkaa mbadala uliofanya baadhi kujiajiri, safari yake haikuwa rahisi. Katika makala iliyopita tulisimulia namna Tausi Msangi alivyojifunza na ambavyo amewafundisha wengine zaidi ya watu 400. 

Leo tunaendelea na safari hiyo na namna unavyoweza kujifunza kutengeneza mkaa mbadala kupitia Tausi. 

Alipopata mafunzo hayo, Tausi hakuanza moja kwa moja kufundisha, alijipa muda ili kupata uzoefu kwanza. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuutengeneza mkaa huo na kutumia nyumbani kwake.

“Sisi tulianza kutengeneza kwa mikono tunatumia wenyewe majumbani, tukaona tunaweza baadaye tukaanza kutoka kwenye kata tofauti tukiwafundisha watu,” anasema mtaalam huyo wa mkaa mbadala.

Awali alianza kutengeneza kwa mikono kwa sababu hakuwa na mashine baadaye akaanza kuwauzia majirani zake na kujipatia kipato kidogo. Uzoefu alioupata na kuongezeka kwa kiu ya watu kujua kuhusu mkaa huo kulimuongezea kasi ya kuwafikia watu wengi zaidi.

“Nilipojifunza kuhusu mkaa huu niliachana na mkaa wa kawaida. Nyumbani kwangu tunatumia huu mkaa, wakati wa kufundisha mimi nakua shuhuda namba moja kwa sababu nimeutumia kwa muda mrefu,” anasema Tausi huku akitabasamu.

Haikua rahisi kukubalika kwenye jamii

Wakati anaanza kuzunguka mitaani kutoa elimu hiyo wengi walikuwa hamuelewi lakini hakukata tamaa.

“Kwanza mwanzoni watu walikua hawaamini kama ule unaweza kuwa mkaa, ilikuwa ni changamoto. Unaenda mahali unawafundisha watu ukienda kufuatilia matokeo unakuta hamna aliyefanya,” anasema Tausi.

Waliomwelewa walienda naye na kutumia maarifa yake kuwafundisha wengine. Taratibu somo likaeleweka kwenye jamii hasa Kipunguni ambapo kaya nyingi zinatumia mkaa huo. 

“Tulipokuwa tukienda tukiona matokeo hakuna tunawarudia tena hata kwa viongozi wao wa mtaa wanatukusanyia watu tunafanya tena darasa lingine walau kidogo kidogo watu wakaanza kuelewa,” anasema.

Zaidi ya robo tatu au asilimia 88.2 ya kaya zilizopo Jijini Dar es Salaam zinatumia mkaa wa kawaida kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mapishi.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati ya mwaka 2019/20 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) asilimia 70 ya mkaa unaozalishwa nchini kutumiwa na wakazi wa Dar es salaam.

Ikiwa mkaa mbadala utapewa kipaumbele basi utasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa.

‘Wanaume waninichukulia poa…ni ajira’ 

Tausi anasema licha ya kukubalika zaidi na wanawake wenzake, wako baadhi ya wanaume akisimama mbele kufundisha kuhusu mkaa mbadala humchukulia poa wakidhani hawezi kutoa maarifa yanayoweza kubadilisha maisha yao.

Licha ya changamoto hizo, wito wa kufundisha hajauacha kwa sababu lengo lake ni kuwasaidia wanawake kuboresha maisha kupitia mkaa mbadala.

“Mimi mwenyewe ni mhanga wa mimba za utotoni, maisha magumu niliyoishi sipendi mabinti wapitie, hata kama nitakutana na changamoto lazima niwasaidie wajiajiri kwa mkaa mbadala na shughuli ndogo ndogo ili kuwapunguzia umaskini,” anasisitiza shujaa huyo wa nishati safi ya kupikia. 

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala Kipunguni wakiendelea na shughuli ya uzalishaji. Picha| Esau Ng’umbi.

Mafanikio aliyopata

Ufundishaji ni kazi ya mama huyo. Kupitia kazi hiyo amekuwa akijipatia kipato ambacho humsaidia kuendesha maisha yeye na familia yake. 

Ikizingatiwa kuwa yuko kwenye kikundi cha Sauti ya Jamii, mkaa wanaotengeneza wamekuwa wanauza kwa watu mbalimbali hivyo kujipatia kipato.

“Kwa siku mashine yetu ina uwezo wa kutengeneza tani moja hadi mbili za mkaa,” anasema Tausi huku akitabasamu.

Mkaa mbadala ni maisha

“Wito wangu waachane na masuala ya kukata miti hovyo, kuleta jangwa katika nchi yetu ya Tanzania, waachane na masuala ya kusema bila gesi wao hawawezi kuishi, wajifunze kutengeneza mkaa huu kukidhi mahitaji yao,” anahitimisha Tausi.

Unaweza kuwasiliana na mwalimu wa mkaa mbadala Tausi Msangi kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia namba 0713865804.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa