Sauda Mahita: Msomi anayechagiza nishati safi ya kupikia Tanzania

Na Lucy Samson
12 Aug 2022
Anatunia elimu yake kuwasaidia watu kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo majiko banifu yasiyochafua mazingira.
article
  • Anauza vifaa vya jikoni yakiwemo majiko yanayotumia nishati safi na salama.
  • Ana ndoto za kumiliki kiwanda kichotengeneza bidhaa zisizochafua mazingira.

Siku yake huanza kwa purukushani za asubuhi zilizopo jiji la Dar es Salaam akitokea Tegeta mpaka Kinondoni jijini hapa tayari kuanza majukumu yake ya siku hiyo.

Kwa mwaka mmoja sasa amekuwa akifanya kazi hii ambayo kadiri siku zinavyoenda ndivyo anavyozidi kuipenda na kutamani siku moja amiliki kiwanda kitakachozalisha bidhaa zitakazokuwa mbadala wa bidhaa zinazochafua mazingira.

Ni Sauda Mahita, Afisa Masoko kwenye kampuni ya Smart Mnada inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya kielektroniki vinavyotumia umeme na gesi yakiwemo majiko yanayotumia kiasi kidogo cha nishati ya mkaa ya Eco Zoom.

“Sisi tunauza majiko ya kisasa ,tuna cookware (vifaa vya kupikia) kama majiko haya yakutumia mkaa mchache, majiko ya umeme, pressure cooker (jiko la mvuke) majagi ya kuchemshia maji , tuna pasi na mafriji pia,” anasema Sauda.

Vifaa hivyo vinavyotumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia majumbani vinavyouzwa na kampuni hiyo vimekuwa na mchango mkubwa katika kuwatoa watu kwenye matumizi ya mkaa na kuni na kuanza kutumia nishati safi na salama.

Pia kazi anayofanya binti huyo ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha, kuokoa mazingira na kutengeneza ajira hasa kwa wanawake ambao ni waathirika wa matumizi ya kuni na mkaa.

“Kazi yangu kubwa katika kampuni ya Smart Mnada ni kuhakikisha bidhaaa zetu zinamfikia kila Mtanzania ili kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana matumizi makubwa ya nishati ya mkaa na kuni,” anasema Sauda.

Hata hivyo, hataki kuendelea kuajiriwa maisha yake yote bali ana ndoto ya kufungua kiwanda kitakachokuwa kinatengeneza bidhaa za kupikia zinazotumia nishati safi ikiwemo umeme na gesi ya majumbani (LPG) ili kuwa sehemu ya kuboresha maisha ya jamii yake.

Jiko la Eco Zoom ambalo kampuni anayofanya kazi Sauda Mahita wanauza. Jiko hilo linatumia mkaa kidogo. Picha| Samart Mnada.

Anapenda anachofanya

Sauda ni msomi kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambapo licha kusomea kozi ya Bima na Usalama kwa Jamii alijikuta akiipenda kazi hii ya afisa masoko katika sekta ya nishati. 

Kazi hii ni ya kwanza kwake tangu amalize chuo, bado anaifurahia na kuona matumaini mapana kwenye jamii ya Watanzania endapo wataamua kugeukia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kiukweli kazi hii ni nzuri na ninaipenda, nilivyoanza sikutegemea kama itakuwa kwa ukubwa kama niunavyoona sasa hivi, nina matumaini makubwa endapo tutatumia bidhaa hizi tunaweza kupunguza uchafuzi wa mazingira,” anasema Sauda.

Faida za kutumia nishati safi pamoja na uhitaji wa kutumia bidhaa hizo kulimvutia Sauda kuingia kwenye kazi hii ili aweze kusambaza kwa watu mbalimbali kuwa  nje kidogo ya kile alichosomea chuoni.

“Kwanza sikutegemea kwamba nitakuja kufanya kitu hiki, kilichonivutia ni baada ya kipita mitandaoni nikaona wanachofanya nikapenda kwa sababu ni vitu ambavyo navihitaji na watu  wanaonizunguka wanavihitaji,” anasema Sauda.

Akiwa kama afisa masoko kazi yake nyingine ni kutoa elimu  kwa wateja wake juu ya matumizi ya majiko hayo yanayopunguza matumizi ya nishati ya mkaa lakini bidhaa nyingine za kisasa.

“Watu wengi wanayaelewa majiko lakini wengi wanakuwa hawaamini kwa hiyo tunapata kazi kidogo kuwaelimisha mpaka mtu anapochukua jiko na kulitumia ndio hapo anapata kuelewa,” anasema Sauda.

Kazi hii inalipa? Majiko ya Eco Zoom yanafaida gani? Unawezaje kuanza biashara hii? Usikose sehemu ya pili ambapo Sauda Mahita atafafanua kwa undani.

Unaweza kuwasiliana na Sauda Mahita kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia namba 0686860033.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa