Taka zinavyowaokoa na ukata, tunza mazingira Dar es Salaam

Na Herimina Mkude
1 Apr 2022
Watu waliopo kwenye kikundi hiki sasa wana uhakika wa kipato kwa mwezi kutokana na kazi yao ya kugeuza taka taka kuwa nishati safi ya kupikia.
article
  • Ni juhudi zinazofanywa na kikundi cha Kigilagila Rafiki wa Mazingira za kuzalisha mkaa mbadala kutoka kwenye taka taka.
  • Kikundi hiki huzalisha hadi tandi 2 za mkaa mbadala kwa wiki.
  • Faida wanayoipata yawapunguzia makali ya umaskini.

Dar es Salaam. Kwa kawaida imezoeleka kutupa taka  tunazotengeneza nyumbani ikiwemo mabaki ya vyakula, maganda ya matunda na hata majivu kwa kuwa hazistahili kuwa ni uchafu. 

Hata hivyo, kwa Kikundi cha Kigilagila Rafiki wa Mazingira, taka hizo ni mali baada ya kuzigeuza kama chanzo cha ajira na kujipatia kipato. Kwao taka si uchafu tena bali ni dili.

Safari ya kuzigeuza taka kuwa mali haikuwa rahisi kihivyo. Septemba 7, 2018, Erepidius Nyerere (65) na wenzie 20 waliamua kuanza rasmi safari yao ya kujitafutia kipato kwa kutengeneza bidhaa zitokanazo na taka, ikiwemo mkaa mbadala na sabuni za kufulia baada ya kukwama kimaisha kutokana na kipato kidogo.

Safari ya mageuzi

Katika safari hiyo, waliamua  kugeuza eneo ambalo lilikuwa ni dampo la taka lisilo rasmi  maeneo ya Kigilagila jijini Dar es Salaam na kutengeneza kiwanda chao kidogo cha urejelezaji taka.

“Huku kulikuwepo dampo, takataka zilikuiwa zimejaa hadi kule juu (akionyesha eneo la juu la kiwanda chao) kulikuwa vichakani wanaojidunga madawa (ya kulevya) ndo yalikuwa makao yao,” anasema Nyerere ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi hiki. 

Pamoja na majukumu yao mengine ya kusaka kipato, wanakikundi hao iliwachukua miezi mitatu kusafisha eneo na kujenga kiwanda na shughuli zote hizo walizifanya wenyewe.

Baada ya semina mbalimbali walizopewa ikiwemo kutoka Shirika la Utafiti wa tiba barani Afrika (AMREF), Januari 2019, ilikuwa ni historia kwa kikundi baada ya kuwasha mashine yao ya  kwanza ya kuchakata taka yenye thamani ya Sh15 milioni ambayo walikabidhiwa na shirika hilo. 

Hata pamoja na jitihada za kukamilisha ujenzi kwa wakati, kasi ya safari yao ilikumbwa na vikwazo lukuki ikiwemo kutopokelewa vizuri na soko kwa kuwa ni bidhaa mpya.

Mkaa mbadala ni moja ya nishati safi za kupikia. Utengenezaji wake unaokoa mazingira kwa kuondoa taka mitaani lakini na kuepusha moshi wenye madhara kwa binadamu. Picha|Hermina Mkude.

Namna wanavyozisaka taka

Kikundi hiki chenye watu 12 wakiwemo wanawake saba huzunguka mtaani na pikipiki za kubebea mizigo (Toyo) kukusanya taka ambazo zina tengenezwa majumbani.

Taka wanazozikusanya ni pamoja na maganda ya matunda, mavumbi ya mkaa, maranda ya mbao, majivu pamoja na majani makavu.

Ukusanyaji wa taka huusisha pia kusaka udongo wa mfinyanzi, kazi ambayo hufanywa zaidi na wanawake wa kikundi hiki. 

Baada ya kukusanya taka, huzichambua kwa kuondoa taka ngumu ambazo mashine yao haina uwezo wa kuzichakata ikiwemo misumari na chupa. 

Wanachakataje takataka hizo? 

Hatua ya uchakataji huusisha kuchanganya taka pamoja na malighafi nyingine kulingana na bidhaa wanayotengeneza.

Kwa mkaa mbadala, kikundi hiki  huchukua mavumbi ya mkaa, udongo wa mfinyanzi, uji wa muhogo pamoja taka nyingine na kuvichanganya kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Martha George (43),  ambaye amefanya kazi kwenye kikundi hiki kwa miaka miwili  sasa, wanatumia udongo wa mfinyanzi na uji wa muhogo kufanya mchanganyiko huo kushikana.

Baada ya mchanganyiko kukamilika wanauweka mchanganyiko huo kwenye mashine ambayo hutengeneza  umbo la mche duara. Miche hiyo ya duara huanikwa juani ili kupata mkaa mkavu. 

Wanawake ni nguzo kuu katika mchakato wa uzalishaji wa mkaa mbadala katika kikundi hiki. Kwa wastani huzalisha kati ya tani 1.5 hadi tani 2 kwa wiki. Picha|Hermina Mkude.

Jambo la kuvutia ni kuwa shughuli ya kutoa miche hiyo ndani ya chumba cha uchakataji na kuanika hufanywa na wanawake wa kikundi hiki.

Unaweza hisi kazi hiyo ni rahisi lakini kwa wiki wanawake hawa wanaanika takriban tani 1.5 za mkaa huo.

Wawatoa kwenye umaskini

Licha ya kuonekana kuwa wanachozalisha ni kipya, mkaa mbadala umekuwa ni neema kwa watu hawa.

“Kazi hii inanipa faida nzuri , kuna mikopo huwa nachukua na nailipa kutokana nna hela ya kazi hii, halafu sina haja ya kununua mkaa maana naupata hapa hapa kazini,” anasema Kurwa Joseph huku akitabasamu..

Kikundi hiki huzalisha kati ya tani 1.5 na tani 2 endapo mashine haitapata changamoto huku malengo yao ni kuongeza zaidi uzalishaji siku zijazo.

Baada ya kuzalisha kiwango hicho,  wanunuzi hununua kwa wastani wa Sh500 kwa kilo bei ambayo ni chini ya ule mkaa wa mitaani ambao fungu moja huuzwa Sh1,000. 

Kutokana na wateja wao wakubwa kuwa wauza chipsi, hufanya kwa siku kikundi hiki kuuza kilo 180 hadi 200, hivyo kwa siku kikundi hiki hupata kati ya Sh90,000 hadi Sh100,000 ambazo husaidia kuendeleza shughuli zao kiwandani pamoja na kulipana mishahara. 

Paulina Mwakatika anasema kuwa mkaa mbadala unapendwa sana na watumiaji ikiwemo wauza chipsi kwa sababu hauishi haraka,  hauna moshi na hausumbui kuuwasha.

“Wauza chipsi wanaupenda sana huu mkaa, na hata nyumbani vile ukibandika maharage hadi yanaiva hauongezi mkaa mwingine,” anasema Mwakatika.

Kikundi hiki kina furahia kazi inayofanya, licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo wakati mwingine mashine kupata hitilafu

Tabasamu la kikundi hiki limeongezeka zaidi baada ya kuwa moja ya vikundi vitano ambavyo vimekabidhiwa vifaa vya kurahisha ukusanyaji taka pamoja na mashine mpya, Machi 31 mwaka huu na Shirika la AMREF kupitia mradi wake  wa Taka ni mali.

 Ujio wa mashine mpya utasaidia kikundi hicho na vingine kuzalisha mkaa mbadala  mara mbili zaidi ya sasa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa