Ukosefu wa nishati safi unavyorudisha nyuma wanawake

Na jikopoint
3 Feb 2022
Wanawake wanapata mkwamo katika kufanya baadhi ya shughuli za kiuchumi ikiwemo ufugaji wa kuku zinazohitaji nishati ya umeme.
article
  • Kukosa nishati kunawasababisha wanawake kuwa na uzalishaji mdogo.
  • Hiyo inatokana na kukosekana elimu juu ya nishati mbadala za uzalishaji.
  • Wadu wa nishati washauri matumizi ya biogesi na umemejua.

Pwani. Wakati wanawake waliofikiwa na umeme wakitumia nishati kuongeza uzalishaji katika sehemu zao za kazi, baadhi ya wanawake wa Halmashauri ya Mkuranga bado wameachwa nyuma.

Wanawake hao wanapata mkwamo katika kufanya baadhi ya shughuli za kiuchumi ikiwemo ufugaji wa kuku zinazohitaji nishati ya umeme.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2020 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikishirikiana na Wakala wa umeme vijijini (REA), wananchi wa Mkuranga wamefikiwa na umeme kwa asilimia 85. 

Hata hivyo, siyo wote wameunganishwa na nishati hiyo. 

Hali hiyo inasababisha wanawake kuendelea kutumia kuni na mkaa ambazo siyo rafiki kwa mazingira na afya zao katika upishi na uzalishaji wa bidhaa.

Licha ya kuni na mkaa kuwa nishati zinazotegemewa zaidi na watu Tanzania, zitajwa kuwa ni chafu na zenye athari kubwa kwa mazingira na afya hasa kwa wanawake ambao wanajihusisha nazo muda mwingi.

Kukosekana kwa nishati kunaweka ukomo katika uzalishaji wa wanawake. Picha| Gift Mojoe.

Miongoni mwa wanawake ambao wameathirika na matumizi ya kuni na mkaa ni wale wanaoishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mtaalamu wa jinsia na nishati kutoka Mtandao wa Nishati na Jinsia Tanzania (Tangsen), Gisela Ngoo amesema katika mgawanyo wa majukumu kijamii, jukumu la kupika ni la mama huku jukumu la kipato likiwa ni la baba.

“Tunapozungumzia masuala ya nishati, anayekata kuni ni mama, anayekoleza mkaa ni mama hivyo, athari za matumizi ya nishati chafu zitamkuta mama zaidi,” amesema Ngoo wakati wa mkutano wa nishati uliowashirikisha madiwani wa Mkuranga na Tangsen wiki hii. 

Hali hiyo inasababisha adha mbalimbali ikiwemo muda mwingi wa kuandaa chakula ikilinganisha na mtu anayetumia nishati safi kama umeme na gesi.

“Kwa anayetumia gesi anabonyeza tu batani na jiko linawaka. Kwa anayetumia kuni, aziandae, aweke mafuta ya taa, awashe na asubiri moto ukolee ndiyo aanze kupika,” amesema Ngoo.

Utafiti uliofanyika katika nchi za Afrika magharibi mwaka 2020 na Onyinyechi Bede-Ojimadu pamoja na Orish Orisakwe unaonyesha ya kuwa, katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, takriban asilimia 83 ya wakazi wake wanatumia nishati ya kuni, makaa ya mawe, mabaki ya mimea na mkaa.

Ripoti hiyo inaeleza pia, kwa matumizi ya mwaka, Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (NKJS) zinatumia nishati chafu mara mbili hadi tatu zaidi ya kanda zingine duniani.

“Kati ya takriban watu bilioni 2.8 katika nchi zinazoendelea wanaotazamiwa kutegemea nishati ya kuni hadi mwaka 2030. Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika pekee zinajumuisha asilimia 33.2 (watu milioni 918) ya idadi yote,” inasomeka ripoti hiyo. 

Wanawake wa Mkuranga pia wanahusika katika shughuli mbalimbali za kuingiza kipato kwenye ngazi ya familia ikiwemo ushonaji, usindikaji wa vyakula, ufugaji na kilimo.

Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo, Amina Hoja ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, matumizi ya nishati duni yanawafanya wanawake kuwa na uzalishaji mdogo katika shughuli zao za kiuchumi. 

“Wanawake wanatumia muda mkubwa sana katika kuzalisha kwa kuwa nishati wanayoitumia inahitaji muda mwingi kufanya kazi. Mfano kwa wanaotumia kuni kuandaa mafuta ya mawese, huwezi kuwalinganisha na wanaotumia teknolojia za kisasa kama gesi,” amesema Hoja.

Matumizi ya nishati duni yanasababisha uzalishaji mdogo unaochukua muda mrefu. Picha| Mariam John.

Zaidi ni kuwa, ukosefu wa nishati safi hasa umeme kwa wakazi wa Mkuranga unazipatia kikomo cha muda shughuli za wanawake wilayani humo.

Shughuli za ushonaji zitaishia pale jua likizama, vivyo hivyo usindikaji kwenye viwanda vidogo na hata kilimo.

“Kwakuwa wanatumia nishati duni, wanaishia kutokupata faida kubwa,” amesema Hoja katika mkutano huo.

Suluhu ya tatizo la nishati 

Ili kutatua changamoto hiyo kwa wanawake wa Mkuranga, Afisa Mradi kutoka Tangsen, Thabit Mikidadi ameshauri madiwani wa wilaya hiyo kuweka malengo ya kuhakikisha matumizi ya nishati mbadala kwa wanawake ikiwemo biogesi ambayo inazalisha nishati ya kupikia na kuendesha mitambo na mashine za uzalishaji.

“Tutaongea na wadau wa teknolojia hizo ili wapate nafasi ya kuja kuonyesha jinsi bidhaa zao zinavyofanya kazi,” ameahidi Mikidadi.

Amesema ikiwa nishati safi itapewa kipaumbele, wanawake wilayani humo wataongeza kasi ya uzalishaji, wataboresha afya zao na hivyo kuwaongezea kipato cha familia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa