Zabibu ni tunda lenye mvuto wa kipekee linalotumiwa duniani kote kwa njia mbalimbali. Iwe ni kuliwa kama tunda bichi, kutengeneza mvinyo au kukaushwa. Kila mtu na matumizi yake.
Tunda hili dogo liko katika mnyororo wa thamani wa tamaduni za chakula, afya na biashara, likiwa chanzo kizuri cha lishe, nishati na hata kipato kwa wakulima.
Hata hivyo, zabibu hazifanani kwa umbo na muonekano. Kwa nini? Kwa sababu ya utofauti wa mazingira na matumizi yake.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), zabibu zimegawanyika katika makundi makuu matatu: za kutengenezea mvinyo, za kuliwa kama matunda na zabibu za kukaushwa (raisins)
Katika makala hii, utazifahamu aina hizi kwa undani zaidi kuanzia sifa zake hadi matumizi yake halisi.
1. Zabibu za kutengenezea mvinyo
Zabibu hizi huchangamkiwa zaidi kwenye sekta ya uzalishaji wa vinywaji vya pombe, hasa mvinyo mwekundu na mweupe.
Hutumiwa katika viwanda vya mvinyo duniani na hupandwa kwenye maeneo yenye hali ya hewa isiyo na joto kali wala baridi kali na mvua ya wastani
Nchini Tanzania, aina maarufu ni Makutupora nyekundu, Syrah, na Chenin nyeupe. Aina nyingine zinazotumika ni pamoja na ‘Cabernet Sauvignon’, ‘Merlot’, ‘Chardonnay’, Tempranillo na Airén.
Zabibu hizi huwa na tunda lenye juisi nyingi na ganda jembamba. Pia huwa na kiasi kikubwa cha sukari, ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa pombe kwa njia ya kuchachua.
Kwa kawaida, zabibu hizi haziliwi moja kwa moja kwa sababu ladha yake ni kali au chachu hivyo hupitia usindikaji ili kutoa mvinyo wenye ubora wa kimataifa, kulingana na aina ya zabibu na eneo la uzalishaji.
2. Zabibu za kuliwa kama matunda
Hizi ni zabibu zinazopendwa kwa ulaji wa moja kwa moja bila kupitia usindikaji wowote.
Huuzwa kama tunda sokoni na mara nyingi hupatikana katika maduka au masoko ya matunda.
Aina maarufu nchini ni Makutupora nyeupe, ‘Regina’, ‘Black Rose’, ‘Rosso’ ‘Crosso’, na ‘Alphonce Lavallee’.
Aina za kimataifa ni pamoja na ‘Concord’, ‘Niagara’, ‘Everest Seedless’, ‘Edelweiss’, na ‘Bluebel’.
Zabibu hizi huwa na nyama nyingi, juisi kidogo na ganda gumu kiasi, zina kiwango cha chini cha sukari ukilinganisha na zabibu za mvinyo.
Kwa sababu ya muonekano wake wa kuvutia, ladha tamu, na muundo wake thabiti, aina hizi hupendwa na walaji wa rika zote, hususan watoto.
Wakati wa kula huchanganywa na matunda mengine katika saladi au kwa matumizi ya moja kwa moja majumbani.
3. Zabibu za kukaushwa (raisins)
Hizi ni zabibu zinazolimwa mahsusi kwa ajili ya kukaushwa na kutumika baadaye kama kitafunwa au kiungo katika vyakula. Hutumika kwenye maandazi, keki, mikate, pilau na hata chakula cha watoto.
Baadhi ya aina zinazopatikana ni ‘Beauty Seedless’, ‘Ruby Seedless’, ‘Halili Belly’, ‘Kismis Creven’, na ‘Cotton Candy’
Za kimataifa ni pamoja na ‘Black Raisins’, ‘Currants’, ‘Sultanas’, ‘Flame Raisins’ na ‘Golden Raisins’.
Majina haya ya zabibu yametokana na asili ya sehemu zinapopatikana.
Zina umbo dogo, ganda jembamba na hazina mbegu, hali inayorahisisha ukaushaji wake kuwa wa haraka. Baada ya kukaushwa, huwa na ladha tamu zaidi na hudumu kwa muda mrefu.
Raisins hupendwa kwa matumizi ya kila siku na ni chanzo kizuri cha nguvu kwa watoto, wanafunzi, na watu wanaofanya kazi nyingi za kushughulisha mwili.
Wewe unachagua aina ipi ya zabibu?