Bagia za dengu: Mahitaji na jinsi ya kupika

Na Lucy Samson
5 Oct 2022
Pishi hili lina mahitaji machache: unga wa dengu, chumvi kitunguu, na hoho.
article
  • Bagia ni kitafunwa kizuri kwa chai au kifungua kinywa cha asubuhi.
  • Pishi hili lina mahitaji machache: unga wa dengu, chumvi kitunguu, na hoho.
  • Mahitaji mengine ni pamoja na mafuta ya kukaangia na karoti.

Inapofika suala la kupika vitafunwa kwa ajili ya chai ya asubuhi watu wengi huwa wanaumiza vichwa na mwisho huamua tu kupita mtaa wa pili na kununua.

Shida inakuja pale unapochoka vitafunwa vya kununua na hujui cha kufanya. Kama wewe ni mmoja wa wanaopata shida kujipikia vitafunwa vyao wenyewe basi leo tumekuletea suluhisho.

Ni mapishi rahisi ya bagia za dengu unayoweza kupika ukiwa nyumbani. Unajiamulia tu nini unaweka kwenye kitafunwa hiki, achana na zile za kununua zenye pilipili nyingi au vitunguu vingi vinavyozidi ukubwa wa kitafunwa chenyewe.

Maandalizi

Ukishanunua unga wa dengu ambao ndiyo mahitaji ya msingi kwenye pishi hili, uchekeche kwa kutumia chujio au kimjini mjini unaweza kutumia mkono tu kuondoa mabonge bonge ya unga au uchafu mwingine unaoweza kuonekana.

Baada ya hapo andaa kitunguu, karoti, hoho, kisha ukatekate kwa saizi ndogo ndogo.

Andaa bakuli kubwa. Weka unga wa dengu, kitunguu maji, hoho, karoti viweke kwenye bakuli kubwa utakalolitumia kutengeneza mchanganyiko wako.

Ongeza chumvi robo kijiko, vijiko 2 au zaidi vya unga wa ngano kutengemea na kiasi cha unga wa dengu ulichonacho.

Baada ya kuweka viungo vyote ongeza maji  kidogo kidogo huku na ukikoroga mpaka upate mchanganyiko mzito.

Kama unapenda pilipili unaweza ukaikata kata na ukaiweka kwenye mchanganyiko wa unga wa dengu na viungo vingine.

Mchanganyiko ukiwa mzito na viungo vyote vimechanganyika andaa  sufuria au kikaango kwa ajili ya kuchoma bagia zako.

Mafuta yakipata moto chota kiasi kidogo cha mchanganyiko wako kwa mkono au kijiko kisha uweke kwenye mafuta yaliyochemka.

Rudia hatua hiyo kwa mchanganyiko uliobakia kisha ziache jikoni kwa dakika nne mpaka tano huku ukizigeuza geuza.

Zikishapata rangi ya kahawia ziepue na uweke kwenye chombo cha kuchujia mafuta, baada ya hapo bagia zako zipo tayari kwa kula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa