Jinsi ya kupika bagia za kunde

Na Mlelwa Kiwale
5 Sept 2024
Faidika wewe na familia huku ukiweza kuzipika kwaajili ya biashara na kujiingizia kipato.
article
  • Hupikwa kwa kuzisaga kunde kwa kutumia blenda au kuzitwanga kwa kinu hadi ziwe laini.
  • Mbali na kupika kwa ajili ya ndugu, jamaa na marafiki nyumbani kitafunwa hiki kinaweza pia kuwa sehemu ya biashara ya kujiingizia kipato.

Kunde ni miongoni mwa vyakula vya nafaka ambavyo hutumika sana katika aina mbalimbali za mapishi, wapo ambao hutumia majani yake kama mboga ya majani na wengine huzitumia kuandaa aina mbalimbali za vitafunwa.

Miongoni mwa vitafunwa unavyoweza kuandaa kwa kutumia kunde ni bagia ambazo hupikwa kwa mitindo mbalimbali ikiwemo kuzisaga au kuzichemsha kisha kuzikaanga.

Aina zote hizi zimekuwa zikitumika sehemu nyingi huku baadhi ya watu wakizitengeneza na kuziuza kuanzia Sh200 hadi Sh500 kutegemea na mazingira wanapoziuzia.

Kutokana na umuhimu huo hata wewe una nafasi ya kujifunza kuandaa kitafunwa hiki ambacho mbali na kuwaandalia watoto, ndugu jamaa au marafiki unaweza kukitumia kujiongezea kipato.

Tuingie jikoni

Hatua ya kwanza katika mapishi ya bagia za kunde baada ya kuzinunua ni kuzichambua (ziwe zimekobolewa au nzima) kwa lengo la kuondoa uchafu wowote unaweza kuwepo au kuzitenganisha na zile zilizoharibika kisha ziloweke kwenye maji masaa 12 au zaidi ili zilainike.

Baada ya kuhakikisha kunde zimelainika vizuri zichuje maji kisha uendelee na maandalizi ya viungo vitakavyotumika katika pishi hili ikiwemo kitunguu maji, pilipili mbuzi, kotmiri, tangawizi na kitunguu saumu ambapo utaviosha (kwa vinavyohitajika kuoshwa) na kuvikata kata kwa saizi ndogo.

Endelea na maandalizi kwa kuchanganya viungo vikavu na kunde ikiwemo chumvi,manjano,baking soda na vingine unavyopendelea, ongeza viungo vingine ulivyoviandaa awali kisha uvichanganye na usage kwa kutumia blenda.

Kama hauna blenda unaweza kutumia mawe ya asili ya kusagia au unaweza kutwanga na kinu hadi kunde zilainike kabisa na kutengeneza mchanganyiko mzito.

Hatua hiyo ikikamilika bandika mafuta jikoni na yakipata moto anza kuchota bagia kiasi kwenye mkono, tengeneza umbo ulipendalo kisha uzikaange mpaka ziwe na rangi ya kahawia.

Wakati unazikaanga hakikisha moto sio mkali sana ili kuepuka kubabua bagia au kuzifanya zisiive kwa ndani.

Baada ya dakika saba hadi nane bagia zikibadilika kuwa na rangi ya khawia zitakuwa tayari kwa kula. Unaweza kuongeza ladha ya kitafunwa chako kwa kuzitengenezea pilipili ya ukwaju, embe au aina yoyote ile utakayopendelea.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa