Uji wa ngano ni miongoni mwa sehemu muhimu ya lishe katika jamii nyingi nchini Tanzania hata barani Afrika ukitumiwa na watu wa rika zote kama kifungua kinywa au chakula cha asubuhi.
Kinywaji hiki huandaliwa kwa kutumia ngano isiyokobolewa ambayo inasifika kwa wingi wa virutubisho kama vitamini B, vitamini E, madini chuma, shaba, zinki, magnesiamu, kemikali asilia za mimea (phytochemicals) na nyuzi nyingi ambazo husaidia katika mmeng’enyo wa chakula na kupunguza hatari ya matatizo ya njia ya chakula kama vile kuvimbiwa.
Pia uji huu wa ngano unafaa kwa watu wenye kisukari na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) inabainisha kuwa aina hii ya chakula hufyonzwa taratibu kulinganisha na vyakula vingine hivyo kupunguza kasi ya ongezeko la sukari katika damu.
Wakati mwingine kinywaji hiki huongezwa maziwa, sukari, na viungo kama hiliki na mdalasini ili kuboresha ladha.
Tuingie jikoni.
Hatua ya kwanza ni kuloweka ngano katika maji kwa masaa 3 mpaka 5 ili kuifanya ngano kuwa laini kabla ya kupika, kama huwezi kuloweka ngano unaweza kuisaga kidogo katika blenda ili upate mchanganyiko wenye unga.
Baada ya hapo bandika sufuria jikoni changanya maji na unga wa ngano nzima kisha upike kwa moto wa wastani huku ukikoroga mara kwa mara ili kuzuia kushikana au kushika chini ya sufuria.
Ongeza chumvi na sukari kama unataka na endelea kupika kwa dakika 10-15 kisha uweke viungo kulingana na uhitaji wa walaji.
Baada ya hapo weka tui la nazi au maziwa (tumia kimoja wapo) kisha punguza moto na uache uji uchemke kwa dakika nyingine 5-10 ili kuhakikisha ngano imeiva vizuri.
Hatua ya mwisho ni kutoa uji kwenye moto na kuacha upoe kidogo kabla ya kutumika.