Fahamu aina saba za kitimoto

Na Lucy Samson
13 Mar 2024
Jikopoint tumekuandalia aina saba za kitimoto ambazo unaweza kuandaa nyumbani au kuagiza unapotembelea sehemu zinazouza kitoweo hicho.
article
  • Ni pamoja na kitimoto rosti, choma na makange.
  • Nyingine  ni mti mti, dawa ya ukimwi na ‘half london’.

Umeshawahi kujiuliza ni aina ngapi za nyama ya nguruwe inayofahamika  maarufu kama kitimoto umewahi kula hadi leo?

Wakati bado unafiria tovuti ya Taste inayojishughulisha na mapishi inasema kuwa kuna aina zaidi ya 50 za mapishi ya kitimoto ambayo hutegemea na asili au sehemu ambapo pishi hilo linaandaliwa.

Miongoni mwa aina hizo kuna aina chache ambazo pengine zimekuwa maarufu kwa muda mrefu kushinda nyingine hususan nchini Tanzania  ikiwemo kitimoto rosti ambayo hupikwa kwa nyanya nyingi, limao na pilipili kwa mbali kwa wale wanaopendelea.

Kadri siku zinavyoenda ndivyo jinsi ubunifu zaidi unavyoongezeka katika pishi hilo na kuwavutia zaidi walaji ambao hutoboa mifuko yao ili kuweza kununua kitoweo hicho.

Jikopoint tumekuandalia aina saba za kitimoto ambazo unaweza kuandaa nyumbani au kuagiza unapotembelea sehemu zinazouza kitoweo hicho.

  1. Kitimoto choma

Baada ya kitimoto rosti basi aina nyingine inayofahamika na kupendwa zaidi ni kitimoto choma ambayo maandalizi yake huhusisha kuweka viungo kwenye nyama (marinate) vikikolea unahamishia kwenye jiko ambapo utakuwa unaichoma na kuigeuza hadi itakapoiva.

  1. Kitimoto nazi

Licha ya uwepo nazi katika maeneo mengi nchini lakini si wengi  wanafahamu kuwa unaweza kuweka nazi kwenye kitimoto.

Mwishoni mwa mwaka jana Jiko Point ilikutana na muuzaji na mpishi wa kitimoto wa muda mrefu Silas Singoye kutoka Kigamboni ambaye ndiye aliyetuonjesha kitimoto nazi kwa mara ya kwanza.

Maandalizi ya kitimoto nazi hayatofautiani na yale ya na nyama iliyoungwa na nazi, ila katika pishi hili unaweza kuongeza njegere na viungo kadri unavyopendelea.

Kitimoto makange ambayo pia imepewa jina la inbox na mpishi Silas Singoye.Picha|Daudi Mbapani
  1. Mti mti

Katika aina hii ya kitimoto wala hatuweki mti, hii ni aiina tu ya kitimoto ambayo ni maarufu katika baaadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam Chef Nicholas Hiza kutoka Kumbya pub ameiambia jikopoint kuwa pishi ni nyama iliyokatwa kwa saizi ndogo kisha ikachemshwa na baadae kukaangwa na kuugwa kwa viungo mbalimbali.

  1. Dawa ya ukimwi

Wengi wakisikia jina la aina hi ya kitimoto huwa wanashtuka kutokana kuhusishwa na ugonjwa wa Ukimwi ambao unaitishia jamii. 

Pishi hili linahusisha nyama ya mbavu ambayo huchemshwa na kisha kuungwa kwa viungo mbalimbali ikiwemo boga dogo (zucchini) tandoori masala na viungo vingine vingi kadri utakavyopendelea.

  1. Kokoto

Kama lilivyo jina lake, aina hii ya nyama hukatwa vipande vidogo vidogo mithili ya kokoto, huchemshwa kwa viungo mbalimbali vya nyama ikiwemo tandoori masala, na chumvi kisha hukaangwa katika mafuta kwa  muda mchache ili kuikausha.

Tofauti yake na nyama ya kawaida ya kuaanga ni kwamba hii hupitishwa kwenye mafuta kwa muda mchache kushinda ile ya kukaanga ambayo hukaa kwa muda refu.

Mbali na ndizi unaweza kusindikiza kitoweo chako na ugali au chipsi.Picha|Esau Ng’umbi.
  1. Half london

Kama hujawahi kufika ulaya basi ukila pishi pishi jindae kusafirishwa hadi pale London nchini Marekani, usiniulize utafika kwa usafiri gani lakini utamu wa aina hii ya kitoweo utakusafirisha na kukufikisha ndani ya muda mchache tu.

Half London ni nyama ya mbavu ambayo huchemshwa pamoja na viungo mbalimbali vya nyama kisha huungwa na  bamia, nyanya chungu, bilinganya ambavyo kwa pamoja huleta ladha murua inayopendwa na walaji wengi wa kitimoto.

  1. Makange

Aina hii ya kitimoto ni mserereko yani kama hujui aina zote za kitimoto basi usisahau kusema ‘makange’ wakati unatoa oda kwa muhudumu wa chakula.

Kitimoto makange huungwa na viungo kama nyanya, vitunguu na nakshi nyingine nyingi ikwemo mboga za majani ili kuinogesha zaidi.

Hizi ni baadhi tu ya aina za kitkimoto tulizokuandalia, ikiwa umependa aina moja wapo kati ya hizo au unapenda kujifunza zaidi wasiliana na Chef Nicholaus Hiza kwa namba 0710 442312.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa