Fahamu aina tano za tambi

Na Nyendo Mwaja
10 Dec 2025
Pia chakula hiki kimekuwa ni mkombozi hasa kwa watu ambao hawana muda wa kukaa muda mrefu jikoni kuandaa chakula. 
article
  • Ni rahisi kupika, hutumia muda mfupi na huchanganywa na aina mbalimbali za viungo.

Tambi ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa duniani kutokana na urahisi wa kupika na uwezo wake wa kuchanganywa na aina mbalimbali za viungo. 

Pia chakula hiki kimekuwa ni mkombozi hasa kwa watu ambao hawana muda wa kukaa muda mrefu jikoni kuandaa chakula. 

Wewe unatumia tambi za aina gani? Kama umekuwa ukitumia tambi pasipo kufahamu ni za aina gani, basi leo utafahamu undani wa aina za tambi na matumizi yake. 

  1. Spaghetti

Hii ni tambi ndefu, nyembamba, ngumu na yenye umbo la mrija. Tovuti ya The cooking Books inaeleza kuwa spaghetti hutengenezwa kwa unga na maji na hupikwa kwa takribani dakika 8-12 kutokana na aina ya bidhaa ya tambi hiyo.

Tovuti hiyo imeeleza aina mbalimbali za spaghetti:

Spaghetti ya kawaida (Standard Spaghetti): hii hupatikana kwa wingi madukani na hufaa kwa aina mbalimbali za michuzi.

Spaghetti ya ngano (Whole Wheat Spaghetti): hii  ni chaguo bora kiafya kwani ina nyuzi nyuzi (fiber) nyingi, lakini huhitaji kupikwa kwa uangalifu ili isiwe laini kupita kiasi au kugeuka uji.

Spaghetti isiyo na ute wa ngano ( Gluten-Free Spaghetti): aina hii hutengenezwa kwa kutumia mchele, mahindi, au mbegu ndogo ndogo zinazotumika kama mbadala wa mchele zijulikanazo kama ‘quinoa’ na zinafaa kwa watu wasioweza kula ute wa ngano.

Spaghetti Safi (Fresh Spaghetti): hii hupatikana zaidi katika maduka maalumu na huiva haraka zaidi kuliko spaghetti iliyokaushwa.

  1. Penne

Penne ni tambi fupi zilizokatwa kwa mtindo wa pembe. Mara nyingi hutumika kwenye vyakula vya kuoka au mchuzi mzito kwa sababu zinakamata vizuri kwenye mashimo yake ya ndani. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Chief Resources, watu wengi wamekuwa wakiuliza maswali kama, Je, ninapaswa kutumia sufuria ya aina gani kupikia penne ya unga wa nafaka?, Je, naweza kupika penne ya unga wa nafaka kwenye kifaa cha kupashia chakula kutumia kipasha chakula (microwave)?, Inachukua muda gani kupika penne ya unga wa nafaka?

Tovuti hiyo imetoa majibu kwamba penne inafaa kupikwa kwenye sufuria kubwa yenye sehemu ya chini nzito kwa sababu husaidia kusambaza joto na kuzuia chakula kuungua.Pia haishauriwi kupika penne kwenye microwave. Tambi hizi zinaiva kwa dakika 8 hadi 10. 

  1. Fettuccine

Fettuccine kwa Kiitaliano inamaanisha “vifaa vidogo”. Ni tambi maarufu, bapa na nene kutoka katika mapishi ya Kirumi, ambayo hutengenezwa kwa mayai na unga.

Ni pana zaidi kuliko spaghetti na inafaa sana kwa michuzi laini na mizito kwa sababu ya upana wake, ambao husaidia mchuzi kushikamana vizuri kwenye kila uzi wa tambi.

  1. Makaroni

Ni tambi fupi zenye umbo la duara lililopinda. Zinajulikana zaidi katika sahani maarufu ya ‘macaroni and cheese’. 

Pia zinaweza kuchanganywa kwenye supu, nyama, mchuzi na jibini.

Hutumia maji mengi wakati wa kupika ili kuzuia zisishikane. Hutumia dakika 7 hadi 10 mpaka kuiva. 

  1. Tambi za kichina

Hizi hupikwa kwa kukaanga, kuchemshwa au kuongezwa kwenye supu. Zinapatikana katika aina mbalimbali kama ‘noodles’ (tambi) za mayai, za mchele na za ngano. 

Hizi hupikwa kwa dakika 3 hadi 5 kulingana na unene na aina ya ‘noodles’, hutumia maji mengi ili zisiweze kushikana na unaweza ukatumia mafuta ya mzeituni, mchuzi wa soya, mboga au nyama. 

Umevutiwa na aina ipi ya tambi? Basi furahia maisha kwa kula chakula unachopendelea hasa tambi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa