Fahamu mbinu 5 za kupika mchuzi mzito

Na Lucy Samson
6 Jan 2023
Unapata tabu kupika mchuzi mzito? JikoPoint tumekusogezea mbinu tano za kupika mchuzi mzito au rosti kama wengi wanavyoliita.
article
  • Ni pamoja na matumizi ya nyanya, tui la nazi, karanga, viazi mviringo na unga wa ngano.
  • Mbinu hizi zinafaa sana ikiwa una familia kubwa au unauza mgahawa.

Moja kati ya sifa ya mpishi bora ni uwezo wake wa kuhakikisha chakula anachopika kinakuwa na ladha na muonekano mzuri.

Hata hivyo, baadhi ya wapishi wanasahau kuwa uzito wa mchuzi au chakula wanachopika unaweza kuongeza mvuto kwa mlaji, hata ambaye anakitazama tu chakula chako.

Hali hiyo hujitokeza kama mpishi hajui maujanja ya kuufanya mchuzi kuwa mzito, jambo linaloweza kumkosesha wateja kwenye mgahawa au watu wasifurahie chakula chake nyumbani.

Kama wewe ni mmoja wapishi wanaopitia changamoto hiyo usijali, makala haya imekuletea mbinu tano zitakazokusaidia kupika mchuzi mzito.

Weka nyanya za kutosha

Aina nyingi za mchuzi au rosti zinahusisha matumizi ya nyanya, tukianzia mchuzi wa nyama, samaki, kuku, maini na dagaa.

Uwekaji wa nyanya za kutosha kulingana na mboga yako kutakuwezesha kupata mchuzi mzito utakaoongeza ladha na kufanya mboga yako kuvutia.

Hata hivyo, nyanya nyingi si nzuri kwa afya hususan kwa wagonjwa wenye vidonda vya tumbo kama tovuti ya Medical News ya nchini Marekani ilivyoainisha.

Karanga za kusaga mbali na kuongeza uzito kwenye mboga pia zina wingi wa protini na vitamini zinazoimarisha kinga ya mwili. Picha |Jiko Point.

Karanga ya kusaga

Hiki ni kiungo muhimu sana kwenye mboga mbalimbali kama mchuzi wa samaki, au mboga za majani ikiwemo majani ya maboga na kisamvu.

Karanga za kusaga ziwe mbichi au zilizokaangwa huwezesha mchuzi kuwa mzito, unachotakiwa kufanya baada ya kuivisha nyanya jikoni koroga kiasi cha karanga za kusaga na maji kwenye kibakuli kisha uweke kwenye mchuzi wako.

Ili kuepusha mabonge mabonge ya karanga unashauriwa kukoroga mchuzi mara kwa mara mpaka utakapochemka ndipo uachie.

Jambo la kuzingatia kwenye mbinu hii ni kuacha mchuzi uchemke kwa muda mrefu jikoni ikiwa umetumia karanga zilizosagwa zikiwa mbichi, hii itaziwezesha kuiva vizuri.

Tumia tui la nazi

Licha ya kuongeza ladha tui la nazi, husaidia kuongeza uzito kwenye mboga yoyote ya mchuzi.

Iwe nazi ya pakti au nazi ya kukuna zote huwezesha mchuzi wako kuwa mzito na wa kuvutia. Muhimu hakikisha unaikuna na kuichuja vizuri nazi yako  kwa maji machache ili iweze kukupatia tui zito litakalonogesha mchuzi wako.

Kwa upoande wa mboga kama maharage nazi inaweza kuyafanya yawe mazito na ladha tamu. Picha| Shuna’s Kitchen.

Unga wa ngano

Mbali na kutumika kupika vitafunwa aina mbalimbali, unga wa ngano pia husaidia kuongeza uzito wa mchuzi.

Unachotakiwa kufanya ni kukoroga kijiko kimoja au viwili vya ngano kwenye kibakuli kisha umimine kwenye mchuzi wako.

Baada ya kuweka koroga mfululizo bila kuachia mpaka mboga ianze kuchemka. Jambo la kuzingatia ni kuacha ichemke mpaka ngano iive vizuri.

Viazi mviringo

Hiki ni moja kati ya kiungo maarufu kwenye upikaji wa mchuzi. Unafahamu kuwa viazi mviringo vinaweza kukusadia kutoa pishi au mchuzi mzito?.

Kama ulikuwa hujui ngoja nikufahamishe, unapopika mchuzi unaohitaji viazi hakikisha viazi vyako vinaiva sana kiasi vya vingine kuanza kupasuka kisha koroga, utaona mchuzi wako  taratibu unaanza kuwa mzito.

Ikiwa hutaki viazi vyako vipasuke unaweza kuviweka mwishoni lakini ukabakisha kiazi kimoja kilichoiva sana ambacho utakisagia kwenye mchuzi wako.

Kwa kumalizia mbinu zote hizi ziitafanya kazi ikiwa utazingatia kiasi cha maji unayoweka kwenye mboga. Ukiweka maji mengi basi sahau habari ya kupika mchuzi mzito na badala yake mchuzi chururu.

Hakikisha unatumia mbinu hizi kwa kiasi kulingana na wingi wa mchuzi wako na mahitaji ya mboga unayopika.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa