Ni chakula maarufu kaskazini mwa Tanzania. Hutengenezwa kwa kutumia maziwa ya mgando na mahindi yaliyokobolewa na hufadhiwa kwenye kibuyu cha asili.
Loshoroo ni chakula cha asili cha kabila la Wamasai na Wameru wanaopatikana kaskazini mwa Tanzania.
Huliwa na watu wa rika zote. Hata watoto na wazee wasiokuwa na meno wanaweza kula kutokana na uwepo wa maziwa.
Kiasili chakula hiki huifadhiwa kwenye kibuyu ili kisiharibike kwa haraka. Kikihifadhiwa vizuri kinaweza kukaa hata wiki moja bila kuharibika. Kinapoendelea kukaa kwenye kibuyu huwa kichachu ndipo utamu wake ulipo.
Maandalizi
Washa jiko bandika sufuria yenye maji yakishapata moto weka mahindi.
Ongeza maji kila yanapokaribia kuisha ili mahindi yako yaive. Yanaweza kuchukua muda wa saa mbili au tatu.
Mahindi yakishaiva yaipue ili yapoe, yakishapoa weka maziwa ya mgando na uyakoroge, yaache kama dakika tano yajichanganye vizuri hapo yatakuwa tayari.
Baada ya chakula chetu kuwa tayari, unaweza kuhifadhi kwenye kibuyu. Wakati wa kula unaweza kuweka kwenye kikombe au bakuli.