Hapo vipi? katlesi ya viazi mbatata na vitamu

Na Fatuma Hussein
5 Feb 2024
Tumekusogezea hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kuandaa katlesi za viazi vitamu na mbatata unaoweza kuliwa wakati wowote
article
  • Pishi hili linaweza kunoga zaidi likisindikizwa na sharubati, au chai ya viungo.

Umeshawahi kujiuliza ladha utakayoipata baada ya kula katlesi yenye mchanganyiko wa viazi vitamu na mbatata?

Wapishi wengi wamezoea kupika katlesi za viazi mbatata pekee zenye viungo mbalimbali, lakini hiyo haikuzuii kuwa mbunifu zaidi wa pishi hilo.

Wakati ukiendelea kujiuliza sisi tumekusogezea hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kuandaa katlesi za viazi vitamu na mbatata unaoweza kuliwa wakati wowote.

Jinsi ya kuandaa

Menya viazi vyako  vyote kisha kata vipande vidogo kiasi na uvichemshe  jikoni kwa dakika 10 hadi 13 ili vilainkie vizuri. Hakikisha unavichemsha katika sufuria tofauti ili viive vizuri.

Baada ya viazi kuiva viepue, weka katika bakuli safi na unanze kuviponda viazi vitamu peke yake had vilainike kisha hamia katika viazi mbatata.

Kwa upande wa viazi mbatata baada ya kumaliza kuviponda weka maziwa na chumvi kiasi, unga wa mchele na uchanganye kwa pamoja hadi vichanganyike.

Endelea kwa kutengeneza madonge kwa viazi mbatata peke yake na viazi vitamu peke yake kisha changanya kwa pamoja  madonge ya viazi vyote ili upate donge moja, hakikisha si kubwa sana ili liweze kuiva vizuri mpaka ndani.

Hakikisha unakata vipande vidogo vidogo vya viazi wakati wa kuvichemsha ili viive vizuri.Picha|Mkulima Mbunifu.

Rudia hatua hiyo katika madonge yote yaliyobakia kisha andaa mayai kwenye bakuli na uanze kupitisha donge moja moja kwenye maji kisha kwenye chenga za mkate.

Chenga za mkate zinapatikana kwa urahisi madukani au sokoni, pia unaweza kutengeneza mwenyewe nyumbani kwa kukausha mkate na kuusaga.

Katika kumalizia pishi lako pitisha madonge yaliyobakia katika mayai na chenga za mkate, yaache kwa dakika tano yakauke kisha  uanze kukaanga kwa moto wa saizi  ya kati.

Kaanga kwa dakika mbili  au tatu mpaka pale utakapoona madonge yako  yamekuwa na rangi ya kahawia, hapo yatoe chuja mafuta na katlesi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Pishi hili linaweza kunoga zaidi likisindikizwa na sharubati, au chai ya viungo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa