Vitumbua ni moja ya vitafunwa pendwa nchini Tanzania. Wengi wamekuwa wakitumia katika mlo wa kifungua kinywa na wengine hula wakati wowote wanapojisikia.
Umaarufu wake bila shaka unatokana na ladha yake tamu na wakati fulani mtu anaweza kughairi kupata kifungua kinywa kwa sababu tu kakosa vitumbua.
Sasa usiwe miongoni mwao kwani hii leo tutakwenda kuangazia namna unavyoweza kujitayarishia vitumbua vyako nyumbani na ukatumia kama kitafunwa kwa muda uupendao.
Mahitaji
Kwanza unatakiwa kuwa na unga wa mchele, unga wa ngano kiasi, hiriki ya unga, sukari, hamira, maji ya vugu ugu pamoja na mafuta ya kuchomea. Ili kuongeza ladha unaweza ukawa na tui la nazi au mayai ingawa si lazima.
Hatua kwa hatua mapishi
Changanya unga wa mchele, unga wa ngano, sukari, hiliki na hamira uvuruge mchanganyiko huo kwa kutumia maji ya vuguvugu mpaka uwe mwepesi kiasi cha kuchoteka na upawa (unaweza kutumia tui la nazi badala ya maji kwa ajili ya ladha).
Ikiwa unataka kuongeza uzito wa mchanganyiko wako unaweza kutumia mayai kulingana na wingi wa mchanganyiko uliopo.
Uache mchanganyiko kwa muda wa nusu saa hadi saa moja kulingana na ubora wa hamira ili uumuke vizuri.
Weka kikaangio cha vitumbua motoni ili kipate moto, kisha utaweka mafuta kwenye vijungu vya kukaangia vitumbua, mafuta yakishachemka unaweka mchanganyo katika kikaangio.
Kaanga vitumbua kwa kutumia moto wa wastani ambapo utasubiri mpaka rangi ya kahawia ianze kuonekana kwa chini ndipo utageuza kitumbua upande wa pili ili kiive.
Ukishatoa kitumbua unapaswa kunyunyiza kiasi cha mafuta kwenye kikaango ili kuendelea kuchoma vingine mpaka mchanganyiko wako utakapoisha kabisa.
Unapoipua weka sehemu ambayo itaruhusu vitumbua kuchuja mafuta,ukimaliza kukaanga unaweza kuendelea kula kwani hunoga zaidi vikiliwa wakati bado vya moto
Unaweza kula vitumbua na maziwa, chai, kahawa, juisi au soda.
Je na wewe unapenda vitumbua? Umewahi kupika? Tuambie kwenye maoni!