Ijue teknolojia safi ya kuchoma nyama, samaki

Na Mariam John
29 Nov 2021
Kuchoma nyama kwa oven badala ya mkaa kunaondoa ladha ya moshi kwenye mboga hiyo.
article

  • Inarahisisha mapishi ya vyakula vilivyokuwa vikipikwa kwa mkaa na kuni.
  • Ni teknolojia salama kwa afya na mazingira.

Imezoeleka kuwa nyama choma lazima ipite kwenye mkaa au kuni lakini hii ni karne ya 21. Mambo yamebadilika.

Katika upishi hasa ule wa kubanika na kuchoma nyama, matumizi ya majiko ya kisasa ndio habari ya mjini kwa wapishi wengi kwa kuwa gesi na umeme vimethibitishwa katika kuongeza ufanisi wakati wa kupika ikilinganishwa na nishati nyingine.

Mkoani Mwanza, kwa sasa hoteli na magenge mengi ya kuchomea nyama na chipsi yanatumia majiko ya kisasa yanayoendeshwa kwa nishati ya gesi na umeme katika upishi wa vyakula hivyo.

Miongoni mwa wapishi, wapo wanaodai kuwa majiko ya kisasa yanasaidia kupika chakula na kikaiva kwa muda mfupi lakini pia wanaepukana na magonjwa yanayoweza kujitokeza kwa kutumia moto mkali kama mkaa na kuni ikiwemo changamoto za mfumo wa hewa na uoni hafifu.

Muuzaji wa majiko ya Kisasa jijini Mwanza, Magreth Magreth anasema ni miaka sasa hajui bei ya mkaa wala kuni katika upishi wake. Kwa Magreth, ujio wa majiko ya kisasa ni unamfanya afurahie upishi wake.

Kwa Magreth, kutumia jiko la umeme lenye ‘oven’  (jiko maalum la kuoka au kuchoma vyakula) anaweza kufanya kila kitu na kwa muda mfupi na unakuwa na uhakika wa chakula kilichoiva vizuri bila harufu ya moshi.

Mama huyo anaeleza kwa sasa anauhakika na kuimarika kwa afya ya ngozi yake na kifua dhidi ya moshi na moto mkali ikilinganishwa na awali.

“Kutumia jiko la gesi au umeme kwenye kubanika nyama ni rahisi, unakomboa muda wa kubanika mboga na inakuwa haina harufu ya moshi kama zile wanazochoma kwenye mkaa au kuni,” anasema Magreth.

Hii ni moja ya teknolojia rahisi inayoweza kuwasaidia wengi kuchoma nyama ndani ya muda mfupi kwa kutumia umeme badala ya kuni. 

Kupitia jiko la umeme, unaweza kuchoma nyama, samaki na kuoka keki. Picha| Bahati Kitchen.

Kupitia majiko hayo, mpishi anaweza kuongeza na kupunguza moto kiurahisi wakati akipika chakula chake, jambo ambalo ni tofauti na mkaa au kuni.

“Sasa wanaotumia mkaa mara unakolea anaaza kupunguza, mara haujashika vizuri. Ni usumbufu,” anaeleza Magreth.

Majiko ambayo yana oven huuzwa kwa bei tofauti tofauti dukani hapo, yapo yanayoanzia Sh290,000 jiko dogo na kubwa ambalo huuzwa Sh790, 000.

Chips kwa gesi, huduma fasta

Kwa jijini Mwanza, kuna vijiwe vingi vinavyotumia gesi kama nishati ya kupikia. Kati ya vijiwe hivyo ni Salimacone kilichopo mtaa wa uhuru.

Mchoma chipsi wa kijiwe hicho, Martine Amos anasema kabla ya hapo alikuwa anatumia mkaa kitendo ambacho kilichukua muda mrefu na kuchelewesha wateja hivyo baadaye kuhamia kwenye gesi.

“Kwanza haichukui muda. Mteja ukimwambia dakika tano chakula tayari ni tano kweli hatupotezi muda wa mteja,” anasema Amos.

Kwa dakika kadhaa ambazo Jiko Point ilitumia ikiwa kwenye kijiwe hiki, ilishuhudia idadi kubwa ya wateja wakihudumiwa kwa muda mfupi ikilinganishwa na sehemu nyingine na wateja walikuwa wengi pia.

Mteja aliyefika katika kijiwe hicho, Neema Cosmas anasema chakula chao ni kisafi na hakitumii muda mrefu kuandaliwa.

“Hapa kama una haraka unahudumiwa na kuwahi unakoenda tofauti na sehemu nyingine,” anasema Cosmas.

Mbali na kero ya moshi wakati wa kupika, kuchoma nyama kwa mkaa kunahitaji uangalizi wa karibu wakati wa kupika. Picha| Ashiki wa Kiswahili.

Imani ya muda inavyokwamisha biashara

Mchoma chipsi karibu na uwanja wa mpira wa Nyamagana, Joseph Mallya anasema katika kipindi chote cha kazi yake, ametumia mkaa jambo linalomfanya aamini kuwa ni nishati pekee inayoweza kumsaidia kufanya biashara wakati si kweli. 

Mallya, ambaye amekuwa katika biashra hiyo kwa miaka 10 sasa,  hufika kijiweni kwake alfajiri akiwa na vitu vyake ya kuchomea nyama na kuandaa mkaa ambao hutumia hadi dakika 20 kukolea kabla ya kuanza kazi. 

Hii ni tofauti na watumiaji wa gesi kama Amos ambaye hutumia dakika chache kuanza kuandaa chakula. 

Mallya hutengeneza mishikani 100 kwa siku ambapo kila mshikaki mmoja huuza sh 500. Pamoja na hayo, hutengeneza chipsi pia.

Mpishi huyo anasema uchomaji wa mishikaki kwa kutumia mkaa unarahisisha nyama kuiva vizuri kwa kuwanyama isipoiva hadi ndani husababisha matatizo ya kiafya kwa mtumiaji kama ugonjwa wa magoti na gauti.

Anasema uchomaji wa nyama unafaa kwenye moto unaowaka kama mkaa au kuni za kawaida ili kuifanya iive vizuri na si kuibabua kwa nje.

Kuchoma nyama kwenye jiko linalotumia mkaa huacha mboga hiyo ikiwa na harufu ya moshi. Picha| BBC.

Anakiri kuwa teknolojia imerahisisha katika suala nzima la upishi lakini pia anadai itachangia katika kuongeza magonjwa yanayosababishwa na chakula kutoiva vizuri jambo ambalo si kweli. 

Huenda Mallya hajapata elimu juu ya uwezo wa majiko ya nishati safi kupunguza na kuongeza moto kulingana na mahitaji ya mtumiaji.

Nishati safi kama gesi na umeme husaidia kutunza mazingira na kuokoa gharama za kifedha hasa wanaohitaji kiwango kikubwa cha nishati ya kupikia kama Mallya na Amos.

Hatari kwa wanaotumia mkaa, kuni

Matumizi ya nishati ya kuni na mkaa katika upishi kwa mujibu wa wataalamu wa afya yanasababisha matatizo mbalimbali za kiafya ikiwemo saratani ya ngozi, uoni hafifu na magonjwa ya mapafu.

“Ninachokifanya nikitoka hapa kwenye moto nikifika nyumbani sharti la kwanza ni kuoga maji ya baridi, ukiacha kuoga unaweza kuanza kuhisi baridi ,”anasema Mallya.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa