Je, huwa unapika hoho kiusahihi?

Na Herimina Mkude
27 Jan 2022
Inashauriwa kuziweka baada ya mboga yako kuiva ili zibaki na virutubisho ambavyo ni muhimu kwenye mwili wa binadamu.
article
  • Kiungo hiki chenye utajiri wa madini chuma hakitakiwi kuiva sana kwenye mapishi
  • Unashauriwa kuipika mwishoni baada ya mboga kuiva.

Dar es Salaam. Katika mapishi ya kila siku pilipili hoho ni moja ya kiungo au hitaji la muhimu.

Japo huwa tunakichukulia kama kiungo tu, pilipili hoho ipo katika kundi la mboga za matunda, ila kwa tuliozowea kuliita kiungo, na tuendelee hivyo hivyo.

Mbali na kuleta harufu nzuri, kiungo hicho huongeza ladha tamu katika pishi hasa katika mboga za mchuzi.

Hata hivyo, wengi wetu tumekuwa tukikipika kiungo hicho visivyo, hapa naamanisha huwa  tunakipika tofauti na inavyotakiwa.

Wewe huwa unapikaje? 

Kwa mazoea, wengi huwa tunaanza kuweka viungo mbogamboga namaanisha, kitunguu, karoti na hoho mwanzoni mwa pishi letu, kitu ambacho kitaalamu hairuhusiwi.

Uwekaji wa viungo kama hoho ambayo ni rahisi kuiva mwanzoni mwa pishi hufanya kiungo hicho kuiva sana na hivyo kusababisha virutubisho kupotea. Hata ladha yake, siyo poa.

Kabla hatujaenda kwenye namna sahihi ya kupika  pilipili hoho, ngoja nikufahamishe baadhi ya faida za kula kiungo hiki.

Pilipili hoho ina utajiri wa madini chuma hivyo ina umuhimu mkubwa katika afya zetu. Inasaidia kupunguza uwezekano wa magonjwa yanayosababishwa na upungufu wa madini hayo ikiwemo upungufu wa damu.

Kiungo hiki pia kina wingi wa vitamin C ambazo ni muhimu katika afya ya macho.

Hayo yote utayakosa endapo utakipika ndivyo sivyo kiungo hiki na kuishia  kula ‘makapi tu’.

Pilipili hoho zinakuja na rangi tofauti. Picha| Masterclass.

Namna sahihi ya kupika pilipili hoho

Hatua ya kwanza ni kuandaa kiungo hiki kabla hujakipika, na hapo utaanza kwa kuiosha hoho vizuri na ukate sehemu ya juu (‘sterm’), kisha ikate katika vipande viwili.

Baada ya hapo toa mbegu zote, japo ulaji wa mbegu hizo hauna madhara lakini mara nyingi huleta ladha ya uchungu kwenye pishi.

Kata hoho katika vipande vya kawaida usikate vidogo sana, kwani vitawahi kulainika.

Hadi hapo hoho ipo tayari kwa kupikwa. Na hapa ndipo umakini unahitajika.

Jambo la kwanza la kuzingatia, ni kuwa katika mapishi ambayo yanatumia muda mrefu kama pilau na  mchuzi, hakikisha hauweki hoho mwanzoni mwa pishi lako.

Subiri hadi pishi linavyokaribia kuiva  ndipo uweke hoho, na ukishaweka usiache ikae sana jikoni.

Ili ujue kwamba hoho yako umeipika kiafya, wakati unapokula utauhisi ugumu ugumu wake kwani inakuwa haijaiva sana.

Najua inaudhi kula hivyo lakini nikusihi uvumilie kwani ndiyo afya yenyewe na ukiendelea kufanya hivyo utazoea tu.

Kiungo hiki ‘kinanoga’ katika mapishi mengi ikiwemo  nyama, tambi, pamoja na pilau.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa