Je unatafuta chakula cha haraka haraka kitakachowavutia, wageni na wale uwapendao? basi shawarma ni ndiyo yenyewe.
Ikiwa hufahamu shawarma ni pishi linaloandaliwa kwa kutumia mchanganyiko wa viungo mbalimbali pamoja na nyama ambayo inaweza kuwa ya kuku, mbuzi, ng’ombe au kondoo.
Shawarma ni chakula cha asili ya mashariki ya kati, na historia yake inahusiana na tamaduni za Kiarmenia, Kituruki na Kiarabu ingawa ni maarufu nchini Uturuki, Lebanon, na Syria.
Chakula hiki huliwa wakati wote na mara nyingi hupatikana katika migahawa mikubwa kuanzia Sh6,000 hadi Sh18,000 kutegemea na aina ya shawarma.
Hata hivyo, unaweza kuandaa msosi huu nyumbani kwako ukiwa na mahitaji pamoja na viungo unavyovipendelea kwa namna rahisi tu, hivyo fyatana nami mpaka mwisho wa makala hii.
Jinsi ya kuandaa
Hatua ya kwanza ni kuandaa nyama ambapo inaweza kuwa ya kuku, ng’ombe, mbuzi au kondoo.
Hakikisha unaosha aina yanyama uliyochagua na kuikata vipande vidogo vidogo ili iweze kuiva kwa haraka
Endelea kwa kuongeza viungo upendavyo ikiwemo limao,chumvi, vitunguu saumu, pilipili manga kisha changanya vizuri na uache viungo vikolee kwa dakika 20 au zaidi.
Baada ya hapo andaa pilipili hoho, kitunguu maji na karoti, menya kisha kata vipande vidogo kwa karoti na kitunguu na uweke pembeni na kwa upande wa pilipili mboga vipande virefu na vipana ndio hupendezesha zaidi shawarma.
Kama unatumia jiko la gesi bandika kikaango jikoni na uache kipate moto kwa dakika 3, weka mafuta kiasi, acha hadi yapate moto kisha weka nyama, tandaza vizuri iive kwa dakika 5 kisha geuza ili iive vizuri upande wa pili na endelea kugeuza mara kwa mara ili nyama iive na maji yakauke.
Kama unatumia oveni huitaji kufuata hatua zote unaweza ukarahisisha kwa kuchanganya viungo na nyama kisha mtie kuku kwenye sahani ya kuokea kwa moto wa sentigredi 400 au dakika 30.
Nyama ikiiva epua na ichambue upate vipande vidogo vidogo kisha weka pembeni.
Baada ya hapo hatua ya mwisho ni kuandaa chapati au tanduri chukua unga wa ngano utie ndani ya bakuli safi kisha tia chumvi,mafuta, maziwa kiasi ,hamira, sukari na chumvi kisha kanda unga mpaka uwe laini.
Baada ya kuukanda ufinike na wache uumuke kwa mda wa dakika 30, baada ya muda huo kuisha ufunue na ueke kwenye kibao cha kusukumia chapati moja kubwa kisha kata madonge matatu na uyasukume kwa muundo wa chapati.
Ukimaliza kusukuma choma chapati kwa kutumia wavu wa kubanikia nyama kama unao ila hakikisha unatumia moto mdogo uku hakikisha unazigeuza kwa umakini ili zisiungue.
Hatua nyingine ni kupunguza moto chukua siagi na upake juu ya kila chapati ili zisikauke na jaza nyama ya kuku juu ya chapati au tanduri kiasi upendacho kisha katia katia kwa juu ya kila tanduri nyanya, salad, dania na mwagia tomato sauce.
Mpaka hapo shawarma yako itakuwa tayari kwa kuliwa na pilipili ya kupika au chochote upendacho.