Jifunze kuandaa wali wa asumini

Na Lucy Samson
21 Aug 2025
Chakula hiki hupikwa kwa kuchanganya wali pamoja na viungo vingine ikiwemo hiriki, mdalasini na karafuu, zabibu
article
  • Unaweza kupikwa kwa kutumia mchele wa basmati au mchele wa kawaida.
  • Hupikwa kwa kutumia viungo vingi vinavyoongeza mvuto na ladha.

Kuna aina nyingi za wali ambazo hupikwa kwa staili mbalimbali lengo likiwa ni kubadilisha ladha tofauti na ile iliyozoeleka pamoja na kuwafurahisha walaji.

Katikati ya aina nyingi za mapishi ya wali JikoPoint imekusogea namna rahisi ya kuandaa wali wa asumini au wengine huuita wali wa jasmini.

Chakula hiki hupikwa kwa kuchanganya wali pamoja na viungo vingine ikiwemo hiriki, mdalasini na karafuu, zabibu, korosho, nazi na nyinginezo ambazo huongeza ladha pamoja na harufu nzuri.

Bila kupoteza muda twende pamoja jikoni ambapo tutaandaa msosi huu unaoweza kusindikizwa na mboga yoyote na kuvutia walaji.

Maandalizi

Kama ilivyo katika mapishi mengine ya wali hatua ya kwanza ni kuchambua mchele na kuuosha kwa maji safi kwa ajili ya matumizi.

Endelea kuandaa viungo vingine muhimu kama iriki, mdalasini na karafuu ambapo unaweza kuzitumia nzima au ukatwanga upate unga laini unaoweza kuutumia kupikia.

Wali wa asumini huhitaji vitunguu vingi hivyo unaweza kuviandaa kwa kuvimenya, kuvikatakata kisha kuvikaanga mpaka viwe na rangi ya kahawia, vichuje mafuta na uviweke kando hadi pale utakapohitaji kuvitumia.

Katika sufuria au kikaangio hicho hicho kaanga korosho pamoja na zabibu kavu (kama utazitumia) mpaka ziwe na rangi ya kahawia kisha zitoe na uziweke pembeni zichuje mafuta.

Hatua inayofuata ni kubandika maji ya wali jikoni na yakichemka weka mchele uliokwisha kuosha, chumvi kiasi chako  pamoja na karafuu, iriki, mdalasini pamoja na jani la bay (bay leave) na ufunikie hadi wali utakapoiva.

Ukiiva toa maganda ya hiriki pamoja na vibanzi vya mdalasini (ikiwa haukuvisaga) na ‘bay leaves’ kisha weka mafuta kiasi, kitunguu maji vya kukaanga, zabibu na korosho na uchanganye vizuri.

Kama utatumia mchele wa basmati basi ukiuweka jikoni pamoja na viungo utauacha kwa dakika chache mpaka ukaribie kuiva kisha upunguze maji na kuendelea na hatua nyingine.

Utachukua sufuria nyingine utaweka mafuta kiasi pamoja na vitunguu maji kisha utaweka mchele juu yake utaweka tena vitunguu maji na korosho pamoja na zabibu na utaweka tena wali juu yake kisha utaupika kwa mto mdogo mdogo, kuupalia au kuuoka mpaka uive.

Mpaka hapo wali wa asumini utakuwa tayari kwa kuliwa na hubamba zaidi ikiwa utaliwa na mboga kavu ikiwemo vitoweo kama samaki, nyama au kuku.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa