Jifunze mapishi rahisi ya vikokoto

Na Lucy Samson
17 Feb 2025
Maandalizi yake ni rahisi na mahitaji yote yanaweza kupatikana kwa urahisi nyumbani.
article
  • Maandalizi yake ni rahisi na mahitaji yote yanaweza kupatikana kwa urahisi nyumbani.

Vikokoto! Sio jina geni kwa waliosoma shule za shule za msingi za serikali au maarufu kama ‘kidumu na fagio’

Kitafunwa hicho kinachotengenezwa na ngano kilikuwa sehemu ya kiburudisho kwa watoto na baadhi ya watu wazima kutokana na ladha yake pamoja na urahisi wa upatikanaji wake.

Leo jikopoint imeamua kukurudisha utotoni, kwa kukufundisha jinsi ya kuandaa vitafunwa hivi kwa njia rahisi na mahitaji machache.

Ikiwa utatumia unga wa nusu kilo basi utahitaji iriki ya unga kijiko kimoja, ‘baking powder’ kijiko kimoja, butter vijiko viwili au mafuta ya kawaida ya kupikia kiasi, sukari kiasi,  maziwa robo au nazi, sukari robo kikombe.

Vikokoto vinaweza kuwa sehemu ya biashara inayoweza kuwagtoa wajasiriamali wengi.Picha|Jess Product,

Maandalizi

Anza kwa kuchekecha unga wa ngano ili kuondoa uchafu wowote unaoweza kuwepo kisha uweke katika bakuli kubwa utakalotumia kukandia.

Katika bakuli lenye unga ongeza sukari kiasi, siagi au mafuta iriki na baking powder kisha uanze kuchanganya taratibu huku ukiongeza maziwa kidogo kidogo au tui la nazi.

Ikiwa una mpango wa kutengeneza vikokoto vya biashara unaweza kutumia maji wakati wa kukanda ila hakikisha unaweka kidogo kidogo huku ukikanda.

Endelea kukanda kwa dakika nane hadi 10 mpaka utakapohakikisha ngano imechanganganyika vizuri.Hakikisha unga sio mlaini sana wala mgumu sana ili iwe rahisi kuendelea na hatua ya kukata.

Ukimaliza hapo unaweza kuacha unga kwa dakika 5 hadi 10 kisha ukaanza kukata na kuusukuma ili kuoata umbo la duara kama chapati nene.

Kuna aina nyingi za mikato ya vikokoto ila aina pendwa ni hii ya mshazari au pembe nne.Picha|Food Lovers.

Baada ya ya kuutandaza unga, endelea kwa kukata maumbo marefu membemba kisha baadae utakata tena upate vipande vidogo vidogo kwenye muundo wa kokoto zitokanazo na mawe.

Ukimaliza kukata achanisha vikokoto vyako ili visishikane na iwe rahisi kukaanga.

Hatua hiyo ikikamilika washa jiko bandika mafuta na yakioata moto kidogo weka vikokoto vyako kisha uvikoroge koroge kila mara mpaka vitakapoanza kubadilika rangi na kuwa ya hawia.

Hakikisha hauachii mkono wakati wote wa upishi wa vitafunwa hivi na moto n wastani ili visiungue na kuleta ladha mbaya.

Mapaka hapo kitafunwa chako kitakuwa tayari unaweza kuvifurahia kwa aina yoyote ya kinywaji utakayopendelea au kuviweka katika vifungashio maalum na kuwauzia watu waliokaribu yako.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa