Jinsi unavyoweza kupika zege la viazi vitamu na mayai

Na Lucy Samson
5 Dec 2022
Mahitaji ni viazi vitamu na mayai, kitunguu maji, karoti na hoho na mafuta ya kupikia.
article
  • Mahitaji ni viazi vitamu na mayai, kitunguu maji, karoti na hoho na mafuta ya kupikia.
  • Linafaa kuliwa asubuhi, mchana na jioni.

“Zege” ni moja kati ya chakula pendwa jijini Dar es Salaam na mikoa mingine. Hii ni kutokana na urahisi wa upatikanaji wake na uharaka wa maandalizi.

Kwa lugha rahisi zege ni mchanganyiko wa chipsi za kukaanga na mayai. Pishi hili linaweza kupikwa nyumbani au ukanunua kwenye vibanda vya mtaani.

Usilolijua ni kuwa sio viazi mviringo pekee vinavyoweza kutoa pishi hili, viazi vitamu navyo vinafaa sana kutoa zege.

Leo tuongeze ubunifu kwenye upishi wa zege. Unachotakiwa kufanya ni kufuatana nami kwenye makala hii mpaka mwisho.

Mahitaji

  • Viazi vitamu na mayai 
  • Kitunguu maji, karoti na hoho
  • Mafuta ya kupikia, na kikaango

Maandalizi

Anza kwa kumenya viazi vitamu, kisha uvioshe na kuvikausha maji. Baada ya hapo uvikate duara kwa saizi ndogo ambayo itakuwa rahisi kukaangika kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.

Mahitaji ni viazi vitamu na mayai, kitunguu maji, karoti na hoho na mafuta ya kupikia.
Umuhimu wa kukata viazi kwa saizi ndogo ni pamoja na kurahisisha uivaji wake pamoja na kuwezesha mayai kuchanganyika vizuri. Picha | Pika kidigitali/Youtube.

Baada ya hapo andaa  kitunguu, karoti, pilipili hoho kwa kuviosha na kuvikata kata kwa saizi ndogo.

Pasua mayai kwenye bakuli weka chumvi na uyakoroge mpaka yachanganyike vizuri.

Andaa jiko na ubandike sufuria au kikaango jikoni tayari kwa kukaanga viazi vitamu. Vikaange kwa moto mdogo mpaka viive.

Viazi vikiiva andaa sufuria nyingine ya kukaangia weka mafuta kiasi na uache yapate moto.

Wakati unasubiri yapate moto changanya kitunguu, karoti na hoho kiasi kwenye bakuli la  mayai  na ukoroge mpaka vichanganyike.

Mafuta yakipata moto weka viazi kiasi kwenye kikaangio na uache kwa dakika tatu kisha umimine mayai kiasi na ukaange kwa dakika tano kwenye moto mdogo.

Baada ya upande mmoja kuiva geuza upande mwingine na ukaange tena mpaka vitakapoiva.

Rudia hatua hiyo hiyo kwa viazi vitamu vilivyobaki. Ukikamilisha hatua hizo, chakula kitakuwa tayari kuliwa.

Chakula hiki ni kinafaa kuliwa kama kitafunwa wakati wa asubuhi, mchana au usiku huku kikisindikizwa na juisi, soda au maji.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa