Jinsi ya kuandaa futari ya mihogo na samaki

Na Lucy Samson
22 Mar 2024
Jikopoint imekusogezea namna mpya ya kuandaa futari ya mihogo ya nazi na samaki bila jasho huku ukijihakikishia kupata ladha tamu inayofaa kwa watu wa rika zote.
article
  • Hii  ni namna mpya ya kuandaa futari ya mihogo ya nazi.
  • Utahitaji Oven ya umeme au jiko la mkaa kwa ajili ya kuoka samaki.

Ni kawaida kwa watu waliofunga kufungulia kwa kupata kifungua kinywa kinachoambatana na aina mbalimbali za vyakula na vinywaji. 

Baadhi ya watu huita kifungua kinywa hicho futari hususan waumini wa dini ya kiislamu ambao katika kipindi hiki wapo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Msimu huu ndipo ambapo utakuta mapishi ya aina mbalimbali za futari ikiwemo ya mihogo na samaki ambayo ni miongoni mwa futari maarufu.

Licha ya umaarufu huo Jikopoint imekusogezea namna mpya ya kuandaa pishi hili bila jasho huku ukijihakikishia kupata ladha tamu itakayofaa kwa ajili ya kutumiwa na watu wa rika zote.

Maandalizi 

Tuanze maandalizi ya futari kwa kumenya mihogo, ambapo utahitajika kutoa maganda ya nje, kukata vipande vidogo vidogo na baadae kuiosha.

Endelea kwa kukuna nazi kwa kutumia kibao cha mbuzi au kusaga na  blenda kisha chuja na utengnisha tui jepesi na lile zito. 

Unaweza ukatengeneza  matui mawili au zaidi kulingana na wingi wa nazi na ikiwa unatumia nazi za pakti basi hakuna haja ya kutenganisha matui.

Baada ya hapo washa jiko na ubandike mihogo yako jikoni weka tui la pili, vitunguu na chumvi kiasi, acha ichemke hadi pale tui likikaribia kukauka ndipo uongeze tui la kwanza na uache jikoni adi pale mihogo itakapoiva.

Ikiwa unataka mihogo yako iive bila kuwa na mchuzi mwingi basi utaweka tui la nazi kidogo kidogo mpaka pale utakaporidhishwa na kiwango cha rojo kilichopo.

Ukimaliza kuandaa mihogo endelea na maandalizi ya samaki ambapo utamsafisha kisha kumuwekea viungo kadri unavyopendelea.

Baadhi ya viungo unavyoweza kutumiani pamoja na soya sosi, fish masala, manjano, pilipili manga, mdalasini, kitunguu swaumu, tangawizi, mafuta ya kupikia na pilipili ya unga kiasi kama unapendelea.

Changanya viungo vyote na upake samaki wako kisha uwaaache viungo viingie kwa nusu saa au saa1.

Bada ya viungo kukolea unaweza kuwaoka kwenye ‘oven’ inayotumia umeme au ukatumia moto wa mkaa, pia unaweza kuwakaanga au kuwachemsha ukatengeneza supu tamu itakayosindikiza mihogo uliyoiandaa

Ukifika hapo utakuwa umemaliza mapishi ya futari ya mihogo na samaki kinachobaki ni kujipakulia na kufaidi utamu unaoweza kusindikizwa na uji au chai.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa