Januari ndiyo hiyo inaishia na mwezi mpya uliopewa jina la “mwezi wa mapenzi” ndiyo unaanza hivyo siyo mbaya ukijiweka sawa na kuandaa vitu vitamu kwa ajili ya uwapendao.
Jikopoint kama ilivyo kawaida yetu kila siku ni siku ya kujifunza na leo tutaandaa kashata za nazi.
Najua utajiuliza kashata za nazi zinahusianaje na mwezi wa mapenzi, lakini nikufahamishe ya kwamba unaweza kuongeza pishi hili katika orodha ya ‘mapocho pocho’ utakayowaandalia uwapendao katika siku ya wapendanao.
Unaweza ukaziandaa mezani kabla au baada ya chakula huku ikisindikizwa na kahawa au kinywaji chochote utakachopendelea
Bila kupoteza muda tuingie jikoni kuandaa pishi letu lenye mahitaji machache ikiwemo sukari, iriki, vanila, nazi pamoja na rangi ya chakula
Maandalizi
Tuanze maandalizi ya pishi hili kwa kuandaa nazi, ambayo unaweza kuikuna kwa kutumia kibao cha mbuzi au ukatumia vifaa vya kisasa kama blenda ili upate machicha ambayo ndiyo hitaji la msingi.
Baada ya hapo washa jiko kisha ubandike sufuria jikoni na ikipata moto weka kikombe kimoja cha sukari pamoja na kikombe kimoja cha maji na ukoroge hadi itakapochemka na kutengeneza mchanganyiko mzito (shira)
Ili kujiridhisha kama shira yako imekuwa nzito kiasi cha kutosha utaiweka kwenye vidole viwili vya mkono na kupima kama vinanata ukivigusanisha, ikiwa havinati basi unatakiwa kuendelea kuipika sukari jikoni,
Wakati huo sukari inaendelea kuchemka na kuwa nzito unaweza kuongeza rangi ya chakula, iriki au vanila ili kuongeza ladha, ikiwa haupendelei basi usiweke.
Shira ikiwa nzito kiasi cha kutosha weka nazi iliyokunwa au kusagwa na kulainika vizuri kisha uichanganye mpaka ili ichanganyike vizuri na shira kwa dakika tano au sita.
Changanya mpaka nazi ikolee sukari na kuwa na rangi moja kisha uzime jiko na umimine mchanganyiko wako sehemu ya kukatia (inaweza kuwa sinia, kibao cha chapati au cha kukatia viungo).
Tandaza mchanganyiko wako kwa kutumia mwiko au upawa ukitengeneza umbo la pembe nne. Baada ya hapo uanche upoe kwa dakika tano na uanze kukata maumbo (pembe tatu au pembe nne) kadri utakavyo na uache iendelee kupoa kwa dakika nyingine 20.
Baada ya muda huo kashata yako itakuwa imepoa na kushikana vizuri hivyo maumbo uliyokakata yatatoka kiurahisi bila kushikana yakikuruhusu kuhamishia katika chombo kingine utakachotumia kupelekea mezani.
Mpaka hapo kashata za nazi zitakuwa tayari kwa kuliwa, unaweza pia kuziweka kwenye friji ili zipate baridi na kuwa tamu zaidi.