Inawezekana umewahi kula aina tofauti za mikate ukiwemo wa jibini, ngano, ndizi, mchele na aina nyingine.
Kitafunwa hiki sio tu kina nzuri lakini kina faida nyingi za kiafya ikiwemo kuongeza virutubisho kwenye mwili kama wanga, protini, vitamini B6, B12, nyuzi nyuzi, pamoja na madini ya selenium, manganezi, fosforazi, shaba na foleti.
Kwa mujibu wa tovuti ya Medicover Hospitals, ulaji wa mkate husaidia kuboresha mmeng’enyo wa chakula, pamoja na unyonyaji wa virutubishi ulioimarishwa.
Basi leo ngoja tujifunze kuandaa mkate wa tangawizi, ambapo kwa baadhi ya watu hupendelea kutumia katika mapishi hususan ya vinywaji kama chai.
Namna ya kuandaa hatua kwa hatua
Hatua ya kwanza katika bakuli kubwa weka unga wa ngano ambao haujakobolewa, unga wa ngano uliokobolewa, chumvi, tangawizi, mdalasini, baking powder na baking soda, maziwa, mayai, mtindi, mafuta ya kupikia na vanilla, kisha changanya mchanganyiko huo. Unaweza kutumia mashine ya kuchanganyia ama mikono kwa dakika 15 hadi 20.
Baada ya hapo chukua sufuria la kuoka mkate, tanguliza karatasi ya kuokea na mimina mchanganyiko wote uliochanganya kwa kutumia mashine ya kuchanganya ndani ya sufuria la kuoka mkate.
Hatua inayofuata ni kuandaa jiko la kuokea mkate. Kwa wale wanaotumia jiko la kisasa la kuokea weka joto la nyuzi 175° C kisha acha jiko lipate moto.
Jiko likishapata moto, weka sufuria la kuoka mkate, na uoke kwa muda wa dakika 40 mpaka 45, au hadi utakapo ona mkate umeiva na kuwa na rangi ya kahawia.
Baada ya dakika 45 utakuwa umesha iva uondoe kwenye jiko la kuoka, kisha uweke pembeni ili upoe, ukiwa bado ndani ya sufuria.
Mpaka hapo mkate wako utakuwa tayari kwa kuliwa unaweza kuula kwa kutumia chai ya maziwa ,viungo ama juisi ni wewe tu utakavyopenda.