Teknolojia imefanya mkate uandaliwe kwa namna tofauti kulingana na mazingira au mahitaji ya mlaji.
Siku hizi kuna mikate ya kukaushwa au ‘toasted bread’ ambayo hupitishwa katika kifaa maalum na kuifanya mikate kuwa na rangi nzuri ya kahawia pia kuna mkate aina ya ‘Sandwich’ ambayo pia huandaliwa kwa aina yake kwa kutumia vifaa maalum.
Licha ya uwepo wa vifaa hivyo unaweza kuandaa sandwich nyumbani kwa urahisi na kuepuka gharama kununua kitafunwa hicho mara mara katika migahawa au hotelini.
Unaweza pia kutengeneza kitafunwa hicho kwa kuwafurahisha uwapendao iwe ni watoto au wageni watakaokutembelea.
Ili kutengeneza kitafunwa hiki nyumbani utahitaji mkate, kitunguu maji, nyanya, tango,parachichi, pilipili manga, siagi, jibini, bila kusahau kikaangio na jiko la kupikia.
Maandalizi
Hatua ya kwanza andaa viungo kwa kuviosha na kuvikatakata kwa umbo la duara kisha kuvihifadhi pembeni.
Baada ya hapo chukua vipande vya mkate (unaweza kutumia mkate wa aina yoyote uwe mweupe au wa kahawia) vipake siagi kisha uwashe jiko na kubandika kikaango tayari kwa kuanza maandalizi ya sandwich.
Kikaango kikipata moto weka siagi kiasi kisha weka kipande kimoja cha mkate.
Anza kupanga viungo kwa kuanzia kitunguu maji, nyanya, tango, parachichi, jibini, pilipili manga na kumalizia kipande cha pili cha mkate ambacho umekipakazia siagi pia.
Hakikisha moto uwe kiasi ili usiunguze mkate huo huku ukiwa unageuza kila upande hadi vibadilike na kuwa rangi ya kahawia.
Ukimaliza epua sandwich ikate kati iwe katika shepu ya pembe tatu na hapo itakuwa ipo tayari kwa kuliwa.
Kitafunwa hiki unaweza kukiandaa muda wowote iwe ofisini, mashuleni, kuwaandalia watoto, familia pamoja na kusukumia kwa kinywaji chochote ukipendacho.