Umeshawahi kusikia kuhusu chapati za hamira zenye mvuto na ladha tamu sawa na chapati za kusukuma?
Ndio kati ya aina nyaiangi za chapati zilizopo duniani chapati za hamira zinaweza kuwa miongoni mwa vitafunwa unavyoweza kuongeza katika orodha ya mapishi yako msimu huu.
Mapishi yake hayatofautiani sana na chapati za kusukuma ila utahitaji kiuongo kimoja zaidi ambacho ni hamira pamoja na dania kama utapendelea.
Pia kwa wafanyabiashara unaweza kuongeza pishi hili na likakuongezea kipato zaidi kwasababu bei ya chapati hizi huanzia Sh1000 kwa chapati hadi Sh1500 katika baadhi ya maeneo.
Chapati hizi hunoga zaidi zikiliwa na mboga mboga kama rosti la maini, supu ya utumbo wa mbuzi au ng’ombe, rosti la biringanya, rosti la kunde, viazi mbatata vilivyoungwa, maharage, choroko ama njegere.
Hivyo, karibu tupike pamoja chapati tamu za hamira.
Hatua kwa hatua namna ya kuandaa chapati za hamira
Anza maandalizi ya chapati za hamira kwa kuandaa unga ambao utauchekecha kuondoa uchafu kisha ongezea hamira, chumvi kiasi, sukari na maji ya vuguvugu na uchanganye kwa dakika tano hadi 10 mpaka utakapoona povu kwa juu ya mchanganyiko ambalo linaashiria kuwa hamira imeanza kufanya kazi.
Katika bakuli lenye mchanganyiko huo changanya unga, maziwa (unaweza tumia mtindi) na mafuta vijiko 4 vya chakula.
Baada ya hapo kanda unga kwa dakika 10-15 hakikisha unachanganya vizuri kwa kutumia mikono au mashine za kukandia unga kama unayo, ongeza maji kidogo kidogo huku ukikanda kisha weka siagi na ukande mpaka ulainike .
Hatua nyingine ni kufunika bakuli la unga kwa kitambaa safi kwa dakika 30 au zaidi mpaka uuumuke ama kuvimba mpaka uwe mara mbili yake.
Baada ya unga kuumuka, sukuma kidogo na ukate vipande vidogo kulingana na ukubwa wa chapati unayotaka unaweza kukata madonge manne mpaka matano.
Tandaza kipande kimoja kwa kutumia mkono hadi kiwe duara, kisha sukuma mpaka kipande kiwe chepesi kiasi.
Hatua inayofuata ni kuweka kikaango jikoni weka chapati ya kwanza na uiche ianze kubadilika rangi kidogo chini, kisha geuza upande wa pili na hapa utachoma kwa moto mdogo mdogo, na ikianza kufura unageuza upande mwingine na kuchoma tena.
Endelea kuchoma hadi pande zote mbili ziwe za rangi ya dhahabu na ziive vizuri pia kumbuka katika upishi wa chapati hizi mara nyingi watu hupika bila mafuta.
Chapati ya hamira inavyoonekana ikiwa jikoni na baada ya kuiva. Picha/ You tube.
Hatua ya mwisho chapati ikisha iva epua na upake siagi pande zote mbili.
Rudia hatua hiyo kwa chapati zote na ukishamaliza chapati zitakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kula na mboga, maharage, au hata chai.