Hakuna kinachovutia zaidi kuliko harufu tamu ya keki iliyookwa kwa ustadi ikiwa na ladha ya kuvutia.
Yote haya unaweza kuyapata ikiwa utaamua kuandaa keki ya nanasi pamoja na na nazi ambapo mbali na ladha pamoja na harufu nzuri aina hii ya keki itakauongezea virutubisho mwilini ikiwemo vitamini C na madini yanayosaidia kuimarisha kinga ya mwili.
Keki hii ni rahisi kuandaa, hata kwa wanaoanza kupika, na inafaa kwa hafla za kifamilia au hata kwa biashara.
Hatua za kuandaa keki ya nanasi na nazi
Maandalizi ya keki hii hayatofautiani sana na keki za kawaida ambapo utaanza kwa katika kuandaa chombo kikubwa kama bakuli ambacho utatumia kuchanganya mahitaji ya msingi.
Anza kwa kuweka weka siagi katika bakuli na sukari kisha changanya kwa kutumia mashine ya mkono au ya umeme mpaka utokee mchanganyiko mwepesi na laini. Hii inachukua takriban dakika tatu mpaka nne.
Kama hauna mashine ya mkono unaweza kutumia mwiko au mchapio kuchanganya mahitaji yote kadri itakavyo hitajika.
Baada ya dakika tano mpaka saba ongeza mayai moja baada ya lingine, huku ukichanganya vizuri baada ya kila yai unaloweka.
Changanya ladha ya nanasi na vanila kwenye mchanganyiko wa siagi na mayai, kisha tia tui la nazi na changanya mpaka kila kitu kichanganyike vizuri.
Badala ya kutumia ‘icing sugar’ unaweza kutumia nazi zilizokaushwa kupambia keki.Picha|Food Network.
Katika bakuli lingine, changanya unga wa ngano, baking powder na chumvi kisha vichanganye mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri.
Ongeza mchanganyiko wa unga kidogo kidogo kwenye mchanganyiko wa siagi, huku ukiongeza maziwa polepole. Endelea kuchanganya kwa takribani dakika 15 hadi upate mchanganyiko laini na mzito.
Hatua inayofuata baada ya mchanganyiko kuwa sawa, unaweza kupaka siagi kwenye sufuria kabla ya kuweka mchanganyiko ulioandaa, au kutumia unga wa ngano.
Ukimaliza hatua hiyo mimina mchanganyiko kwenye sufuria ya kuokea na sambaza kwa usawa, unga wa chini ya sufuria ya kuokea utaifanya keki isishikane.
Washa oveni moto wa nyuzi 175°C (350°F), kisha oka kwa dakika 30-35 au mpaka keki itakapokuwa na rangi ya dhahabu na kijiti kinapochomekwa kitoke safi.
Baada ya kuiva, acha keki ipoe kwa dakika 10 kisha itoe kwenye sufuria ya kuokea na itakuwa tayari kwa kuliwa.
Unaweza kupamba kwa vipande vya nanasi ilokaushwa na nazi uliyoikuna kwa juu baada ya kupamba na sukari ya unga (icing sugar).