Jinsi ya kupika kitimoto nazi

Na Lucy Samson
30 Aug 2023
Kuna aina mpya ya upishi wa rosti ya kitimoto ambayo inaungwa nazi, leo ningependa tujifunze kwa pamoja.
article
  • Ni pishi jipya, hivyo halipatikani sehemu nyingi
  • Inasaidia kuongeza ubunifu kwa wauzaji wa nyama hiyo
  • Ni rahisi kuandaa na unaweza kupika nyumbani 

Nyama ya nguruwe ni miongoni mwa vitoweo vitamu na vyenye walaji wengi duniani kote ambapo kwa hapa nchini Tanzania inafahamika zaidi kwa jina la kitimoto.

Hakuna ushahidi rasmi juu ya maana na historia ya jina hilo ila baadhi ya walaji wa nyama hiyo husema, lilitokana na ukweli kwamba nyama hiyo ikiwa ya moto inakuwa tamu zaidi.

Ni ukweli ulio bayana kuwa utamu wa nyama hii ndiyo unafanya watu wengi kuvutiwa nayo huku watu wengine wakiongeza manjonjo na ubunifu zaidi, ili kuongeza utamu wakati wa kuiandaa hapo utakutana na kitimoto choma, kitimoto rosti, makange na nyingine nyingi.

Kitimoto nazi ni pishi jipya

Aina zote hizo zimezoeleka sana, hauhitaji kueleza maneno mengi kwa wauzaji wakati wa kuagiza, ila kuna hii aina mpya ya upishi wa rosti ya kitimoto ambayo inaungwa nazi, leo ningependa tujifunze kwa pamoja.

Ukiwa kama mpishi unayetamani kuongeza ujuzi huu katika kijiwe chako cha kuuzia kitimoto au unatamani kupika nyumbani kwa ajili ya familia, upo mahali sahihi fuatana nami mpaka pale mapishi ya kitimoto nazi yatakapokamilika.

Tuingie Jikoni

Mapishi ya kitimoto rosti kama ilivyo aina nyingine ya nyama huanza kwa kuchemsha nyama ambayo utaikatakata vizuri utaisafisha na kuiwekea viungo upendavyo.

Unaweza kutumia tangawizi, kitunguu saumu, ndimu pamoja na tandoori masala kuchemsha nyama mpaka iive na kulainika vizuri.

Wakati nyama inaiva, andaa viungo utakavyovitumia ikiwemo kitunguu maji, bilinganya, nyanya chungu, njegere, pilipili hoho, tui la nazi pamoja na pilipili.

Baada ya kumaliza maandalizi na nyama kuiva hatua inayofuata ni kuanza kuiunga nyama kwa viungo na nazi.

Bandika sufuria jikoni mimina mafuta kiasi, yakichemka weka vitunguu na ukoroge hadi vibadilike rangi.

Ongeza nyanya chungu, biringanya, karoti hoho, nyama pamoja na njegere zilizochemshwa, koroga vizuri ili viungo na nyama vichanganyike pamoja.

Dakika Moja au mbili zinatosha kabisa kuchanganya viungo na nyama, hatua inayofuata itakuwa kuongeza maji kiasi na kufunika mpaka viungo vikaribie kuiva.

Viungo vikaribia kuiva huo ndio wakati sahihi wa kuweka tui la nazi, kama unatumia nazi ya kukuna unaweza kutanguliza tui jepesi kwanza kisha ukamalizia na tui zito baadae, lakini kama unatumia nazi ya pakti utaweka yote katika hatua hii.

Tui likichemka vizuri na kutengeneza rojo nzito utaweka chumvi kiasi na hapo kitimoto nazi itakuwa tayari kwa kuliwa.

Msosi huu utanoga zadi ikiwa utasindikizwa na ndizi, chipsi, ugali au chapati.

Je una maujanja mapya ya mapishi ungependa kushea nasi, tupigie kupitia 0677088088 au tuandikie ujumbe kupitia [email protected].

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa