Jinsi ya kupika kitimoto rosti na ndizi za kukaanga

Na Lucy Samson
12 Sept 2023
Katika muendelezo wa mapishi ya kitimoto, leo tunakuletea maandalizi ya kitimoto rosti (inbox) ambayo hupikwa pamoja na mboga mboga, limao na pilipili.
article
  • Ni muhimu kuwa na ndimu au limau kwa wingi
  • Unaweza kuila na ndizi, ugali au hata wali

Kitimoto rosti ni moja kati ya aina maarufu ya pishi la kitimoto inayopendwa na hupatikana katika maeneo yanayouza kitoweo hicho na baadhi hupendelea kujitengenezea wao wenyewe majumbani mwao.

Katika muendelezo wa mapishi ya kitimoto, leo tunakuletea maandalizi ya kitimoto rosti (inbox) ambayo hupikwa pamoja na mboga mboga, limao na pilipili.

Umuhimu wa mboga mboga kama nyanya chungu na biringanya zinazowekwa katika pishi hili ni kutengeneza mchuzi na kuifanya iwe na ladha ya kipekee tofauti na aina nyingine za kitimoto ambazo haziwekwi imbogamboga hizo.

Ili ufaidi utamu wa pishi hili zaidi, basi ni lazima uandae ndimu au limao la kutosha ili kuipa mboga yako utamu zaidi.

Ikiwa unapika mboga hii kwa ajili ya familia au  watoto wasiotakiwa kutumia ndimu nyingi basi unaweza kupunguza au usiweke kabisa lakini hiyo haitaondoa utamu wa pishi la inbox.

Kufahamu hatua za upishi wa mboga hii, basi sogea jikoni tujifunze pamoja

Maandalizi

Hatua ya kwanza ni kabisa kuosha nyama na kuikata katika  saizi uipendayo.

Kisha andaa viungo kama tandoori masala( masala ya mchuzi), tangawizi, chumvi na viungo vingine utakavyopendelea kisha uweke kwenye nyama na uache vikolee (Marination) kwa dakika 20 au zaidi.

Hatua inayofuata ni kuwasha jiko na kuchemsha nyama mpaka iive tayari kwa ajili ya kuungwa.

Wakati nyama inaiva ni muda muafaka wa kuandaa viungo vyako anza  kuosha karoti, hoho, nyanya chungu, bamia na kitunguu maji kisha uvikate kwa saizi ya box.

Katika pishi hili hatutatumia nyanya ila tutatumia biringanya kufanya rosti iwe nzito, kama hauna biringanya unaweza kutumia nyanya kiasi ukipendacho.

Nyama ikiiva anza kuunga kwa kuweka mafuta, kisha pata moto ogeza  vitunguu, vikianza kuiva mimina nyanya chungu, biringanya, karoti na hoho koroga na ufunike kidogo ili viive.

Baada ya dakika tatu mpaka tano unaweza kumimina nyama, koroga ichanganyike na viungo kisha ongeza maji na ufunike ichemke.

Ongeza maji ya limao, chumvi na pilipili kisha uache ichemke mpaka maji yapungue itengeneze mchuzi mzito.

Baada ya hatua hiyo rosti yako itakuwa tayari kwa kuliwa, unaweza kukaanga ndizi mzuzu kusindikiza kitimoto yako. 

Tembelea chaneli ya Jikopoint YouTube uone video mbalimbali za mapishi ikiwemo hili la kitimoto, usisahau kusubscribe na kushea na wengine wajifunze. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa