Wakati mwingine kula kitafunwa aina moja kunachosha, hebu fikiri kama ungehitajika kula maandazi kila siku wakati wa asubuhi ungefanya nini?
Jibu la haraka linaweza kuwa kuongeza nazi kwenye maandazi na kuyafanya yawe matamu zaidi.
Ili ufaidi maandazi haya ni vyema ukaongeza hiriki, kwa hakika harufu na ladha yake itakufanya utamani kukipata kitafunwa hiki katika kila kifungua kinywa.
Ikiwa hujawahi kupika maandazi ya nazi nyumbani usijali upo mahali sahihi, kupitia makala hii utajifunza hatua kwa jinsi ya kuandaa kitafunwa hicho kwa ajili yako au kwa ajili ya biashara.
Shughuli ya mapishi na ianze
Kama ilivyo kwa aina nyingine ya maandazi, hakikisha umeandaa unga wa ngano, hamira, sukari, mafuta (siagi), baking powder (kiungo kinachowekwa kwenye mapishi ya kuoka) pamoja na nazi ambayo tutaitumia leo.
Anza kwa kuchekecha unga ili kutoa uchafu na chochote ambacho kitakuwa kimeingia wakati ukiwa dukani au ndani.
Kisha chekecha unga mimina katika bakuli utalotumia kukanda halafu pima sukari, hamira na baking soda na uchanganye vizuri na unga wa ngano kabla hatujaweka nazi.
Ikiwa hupendi kutumia njia hii, unaweza kupima kiasi kidogo cha tui la nazi, sukari, hamira na baking soda kisha ukasaga na blenda au ukakoroga na mwiko mpaka sukari iyeyuke.
Kwa utakayetumia njia ya kwanza endelea kwa kumimina tui la nazi kiasi kwenye chombo chenye unga kisha uchanganye taratibu huku ukiongeza tui mpaka pale unga utakaposhikana kisha uanze kukanda.
Kanda kwa dakika 20 au zaidi kutegemea na wingi wa unga wako ila hakikisha unga umekuwa laini na hauna madonge.
Paka mafuta au siagi unga wako, kanda tena kidogo kisha ufunike pembeni ili uumuke.
Dakika 30 au 40 zinatosha kabisa unga kuumuka, kabla ya kukata shepu za maandazi kanda tena kidogo ili hewa itoke kisha uache kwa dakika nyingine 10 ndipo uhamie kwenye kukata.
Katika hatua hii maamuzi ni yako, kukata umbo la duara, pembe tatu au pembe nne, ila hakikisha unakata saizi ya kiasi inayoweza kuiva vizuri.
Baada ya hapo washa jiko, bandika kikaango, weka mafuta na uache yachemke kiasi kisha anza kuweka maandazi na ukakaange kwa moto wa wastani mpaka yaive na kuwa na rangi ya kahawia.
Rudia hatua hiyo kwa mandazi yaliyobakia, yaache yapoe kisha yatakuwa tayari kwa kula kwa kinywaji au mboga yoyote utakayopendelea.