Jinsi ya kupika mayai kama kitafunwa au mboga 

Na Lucy Samson
26 Jul 2022
Mahitaji ya kupika kitafunwa hicho ni mayai yenyewe, chumvi na kitunguu maji. Unaweza kuongeza karoti na hoho kama unapendelea.
article
  • Mayai yana vitamin A, vitamin B5 na B12.
  • Ni rahisi sana kuandaa.
  • Utakachohitaji ni kitunguu nyanya na hoho.

Kuna msemo wa Kiswahili unaosema “mchele mmoja mapishi mbalimbali”, leo nataka tuuthibitishe hapa kwenye pishi hili la mayai.

Mayai yanaweza kutumiwa kama kitafunwa cha asubuhi au kama mboga unayoweza kuitumia kwenye mlo wa mchana au usiku.

Kwa mujibu wa jarida la healthline, mayai yana vitamini nyingi ikiwemo vitamin A,vitamin B5, na B12. Pia mayai yana wingi wa protini na omega 3 yenye uwezo mkubwa wa kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.

Kitafunwa au mboga ya mayai ni rahisi sana kuandaa, huchukua dakika tano mpaka 10 kuandaa.

Mayai kama kitafunwa 

Mayai kama kifungua kinywa hufaa pia watu walio katika mpango maalum wa chakula.| Picha CookPad.

Watu wengi hupendelea mayai kama kifungua kinywa au mlo wa asubuhi. Kitafunwa hiki huenda sambamba na mkate, mboga mboga(salad) chapati au kitafunwa chochote unachopendelea.

Mahitaji ya mayai kama kitafunwa ni mayai yenyewe, chumvi na kitunguu maji. Unaweza kuongeza karoti na hoho kama unapendelea.

Maandalizi

Yapasue mayai na uyaweke kwenye bakuli safi kisha ongeza chumvi, na uyakoroge mpaka yachanganyike vizuri.

Washa jiko, weka sufuria au kikaango jikoni, kikipata moto weka mafuta kiasi na kitunguu kilichokatwakatwa. Kikiiva weka mayai na usubiri kidogo kabla ya kuyageuza.

Ongeza hoho na katoti kama unapendelea, baada ya dakika 3 geuza upande mwingine.

Baada ya dakika mbili kitafunwa cha  mayai kipo tayari weka mezani na ufurahie ladha nzuri,

Mayai kama mboga

Mayai yanaweza kuliwa na wali au ugali kwa mlo wa mchana au usiku| Picha Rukia Laltia.

Aina hii ya upishi wa mayai inawafaa sana manbachela na wale wasiopenda kutumia muda mwingi jikoni.

Mahitaji ya pishi hili ni pamoja na nyanya, kitunguu, karoti na hoho.

Maandalizi

Pasua mayai weka kwenye kibakuli koroga mpaka yachanganyike vizuri ongeza chumvi kisha uandae jiko kwa ajili ya kupika mayai.

Weka sufuria jikoni ongeza mafuta kiasi yakichemka ongeza kitunguu maji, kikiiva weka hoho na karoti na ukoroge mpaka ziive kisha ongeza nyanya na ufunike ziive.

Zikiiva na kuchemka vizuri ongeza mayai yako, yaache baada ya dakika mbili na uanze kuyakoroga, rudia kuyakoroga kila baada ya dakika mbili mpaka utakapoona yameanza kutengeneza vidonge vidogo vidogo.

Funika kwa dakika 5, baada yapo mboga yako ipo tayari kwa kula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa