Mbinu za kupika mboga ya mayai

Na Maria Acley
31 Jan 2022
Kupika mboga ya mayai unahitaji viungo vichache. Ndani ya dakika kumi, mboga yako itakuwa tayari.
article
  • Inachukua dakika 10 tu kupika.
  • Mboga hii inalikana chakula chochote.
  • Unachohitaji ni mayai, na viungo vya rosti.

Swali la “nitapika mboga gani” huwa ni gumu sana hasa ukiwa umechoka na unahitaji kupika chakula cha haraka.

Mara kadhaa huwa inatokea ile hali ambayo hujui mboga gani ya kupika na pengine una mchele au unga ndani ila hujui utapika na mboga gani ya haraka , JikoPoint ipo nyuma yako kuhakikisha hauumizi kichwa kabisa.

Miongoni mwa mboga za haraka na zinazohitaji vitu vichache sana kuzipika ni mboga ya mayai ambayo leo tutajifunza na utaifurahia haswa.

Kwakua tunapika mboga ya chap, basi hatuhitaji mambo mengi. Haya ndiyo mahitaji muhimu.

Tufanye maandalizi.

Kwa kuanza, chemsha mayai yako kisha toa magamba yake.

Hatua inayofuatani kutwanga kitunguu swaumu, kata kata kitunguu maji, baada ya hapo andaa karoti na hoho kwa kuzikata kwa maumbo ya urefu.

Tuingie jikoni.

Injika sufuria jikoni kisha weka mafuta ya kupikia, yakipata moto weka kitunguu maji kikaange mpaka kiwe na rangi ya kahawia. 

Baada ya hapo weka karoti ulizoziandaa na ukoroge kwa muda wa sekunde 5 mpaka 6.

Ongeza hoho kisha ukoroge kwa ajili ya kuchanganya vikorombwezo vyako. 

Weka nyanya ya pakti vijiko viwili vya chakula kisha koroga tena ili viungo viweze kuchanganyika vizuri.

Baada ya hapo weka kitungu swaumu na masala kwenye mchanganyiko wako ili kuondoa shombo ya nyanya. 

Unaweza kuongeza viungo vingine ikiwemo majani ya vitunguu maji, na viazi mviringo. Picha| Desi Blitz.

Kwenye aina gani ya masala utumie, unaweza kutumia masala yoyote ya kupikia mboga aidha ya nyama au ya kuku.

Chumvi ni muhimu sana hatupaswi kuisahau, weka chumvi kiasi kisha weka maji robo kikombe na ufunike mboga yako kwa muda wa dakika tano ili kuruhusu viungo kuiva vizuri.

Funua chakula chako, koroga kisha weka yale mayai yako uliyoyachemsha na ukoroge tena kuchanganya mboga yako vizuri.

Na hapo utakua tayari umefanikisha kupika mboga yako kwa dakika kumi tu, pakua mboga yako na waweza kuila na wali, chipsi, ndizi au hata ugali.

Unataka kujua kupika nini tena? Tuulize kupitia +255 677 088 088.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa