Jinsi ya kupika  mboga ya ‘mkunungu’

Na Lucy Samson
5 Sept 2022
Wapo wanaochanganya mkunungu na karanga wakati wa kuutwanga na wengine huweka karanga wakati wa kuupika mara baada ya kuweka nyanya.
article
  • Mboga hii huliwa na ugali
  • Ni rahisi kupika, ina mahitaji machache

Tanzania imebarikiwa aina nyingi za mboga za asili zenye virutubisho vingi vinavyoweza kujenga mwili wa binadamu.

Katika pita pita zangu maeneo ya Iringa nikakutana na mboga hii ambayo wakazi wa mkoa huu huiita “mkunungu”.

Mara nyingi  mmea huo hujiotea tu, kazi kubwa inayosalia ni kuuchuma, kuuanika na kuutwanga ili kupata unga mlaini ambao ndio mkunungu wenyewe sasa.

Wapo wanaochanganya mkunungu na karanga wakati wa kuutwanga na wengine huweka karanga wakati wa kuupika mara baada ya kuweka nyanya.

Nikiwa mkoani humo nilinunua mkunungu wa Sh5,000 ili nisisumbuke kuutafuta tena nikitaka kuupika, ila kwa kawaida mboga hii inauzwa sokoni ambapo kila pakti inauzwa Sh500 au Sh1,000.

Mahitaji

Mkunungu

Mafuta

Chumvi, kitunguu 

Nyanya na maji kiasi.

Maandalizi

Hatua ya kwanza ya pishi hili ni kuandaa mkunungu wako kiasi unachotaka kupika kutokana na wingi wa walaji, hakikisha hauna uchafu wowote wala majani ambayo hayakutwangwa vizuri.

Washa jiko kaanga kitunguu  na mafuta mpaka kiive, kisha ongeza nyanya na ufunike ziive.

Kama ni mara yako ya kwanza kupika mboga unashauriwa uiandae kwa pembeni kwa kumimina kiasi chote cha mkunungu unachotaka kupika na maji kiasi kwenye kibakuli na ukoroge.

Ukorogaji unaotumika hapa ni kama ule wa kukoroga unga na maji kabla hujachangaanya kwenye sufuria ya maji yanayochemka kwa ajili ya kusonga ugali.

Ukihakikisha mchanganyiko wako hauna mabonge bonge changanya na nyanya zako ambazo zimeshaiva jikoni.

Mara baada ya kumimina mchanganyiko wako unatakiwa kukoroga bila kuachia mpaka mkunungu wako uanze kuchemka.

Ukiacha kukoroga kwa muda mrefu mkunungu utaungulia na kupata mabonge bonge. Mkunungu wako ukichemka vizuri ongeza chumvi kiasi na karanga za kusaga na uache mboga yako ichemke.

Ikishachemka  mboga yako itakuwa tayari  kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa