Jinsi ya kupika nyama kwa muda mfupi

Na Rodgers George
6 Nov 2021
Kupika nyama kwenye gesi ni rahisi kuliko wengi wanavyodhani. Unaweza kutumia viungo au vyombo sahihi kufurahia mapishi yako.
article
  • Ni kwa kutumia vyombo sahihi vya kubana mvuke.
  • Unaweza kutumia viungo kama tangawizi na limao.
  • Unashauriwa kuchagua nyama ya mnyama kijana (mdogo).

Dar es Salaam. Huenda ni kati ya pishi linalotia “stress” baada ya maharage. Mara nyingi unatakiwa kupika huku unachungulia ili usiunguze na hapo ndipo shida ilipo.

Mapishi ya nyama yanatakiwa kuchukua makadirio ya dakika 30 hivi kwa mujibu wa wapishi wengi waliozungumza na Jiko Point (www.jikopoint.co.tz) akiwemo Everlyn Oscar ambaye ni Mpishi wa keki kutoka Kinyerezi.

Oscar amesema, “kuna nyama utachemsha dakika kumi itaiva kuna nyingne itaiva nusu saa nyingne hata saa zima na nyingne hata hauchemshi unarost moja kwa moja.”

Hayo yote yanaturudisha kwa Waswahili waliowahi kusema, “mchele mmoja mapishi mbali mbali,” na kila mtu ana njia yake ya kupika nyama.

Hata hivyo kwa njiazote ambazo huenda tumeona mama zetu na dada zetu wakitumia, zipo ambazo zinaweza kufanya nyama isiwe pishi la wewe ambaye unaanza kupika kukimbilia.

Heka heka za kufunua sufuria kuchungulia maji, muda unaoutumia kwenye kupika na mambo mengine mengi yanaweza kukufanya uone ni ahueni uende kwa mama ntilie uagize chakula na sahani uje ikiwa imekamilika.

Leo, nitakwenda kukupatia siri ya kuivisha nyama kwa muda mfupi tena kwa kutummia jiko la gesi au umeme.

Zipo njia zinazoweza kulainisha nyama ikiwemo matumizi ya viungo wakati wa kupika. Picha| BBC Goood Food.

Tumia sufuria la presha

Huenda unadhani ni la kupikia maharage au makande tu kakini haipo hivyo. Sufuria za presha almaarufu kama “pressure cooker” zinaweza kutumika kwenye kupikia nyama na ikaiva kwa muda mfupi.

Sufuria hizi zinakuja kwa saizi tofauti yaani ndogo, kati na kubwa kwa wenye familia za watu wengi.

Sifa kuu ya sufuria hii ni kutokuruhusu mvuke kutoroka wakati nyama inaiva na hivyo kutumia nishati yako ipasavyo na kuivisha nyama ndani ya dakika chache tu.

Mfanyabiashara wa maua na zawadi jijini Dar es Salaam, Irene Albert ameiambia Jiko Point kuwa, kwake anatumia sufuria la aina hiyo na nyama huiva ndani ya dakika kumi tu na hivyo kuokoa gesi yake ikilinganishwa na matumizi ya sufuria zingine.

Tumia viungo

Huenda unavichukulia poa viungo vya tangawizi, limao, na vitunguu swaumu.

Kama haukuwahi kuvifikiria zamani, ni vyema ukajua kuwa viungo hivyo ni muhimu kwenye kulainisha nyama na kusaidia iive kwa wepesi.

Kwa wale ambao hawajanunua sufuria la presha, unaweza kutumia viungo hivi kwa pamoja na hata kimoja wapo kulainisha nyama.

Baada ya kuikatakata, twanga au saga mchanganyiko wa vitunguu swaumu na tangawizi na weka kwenye nyama na kisha pika.

Mbali na kulainisha nyama, viungo hivyo pia vitaongeza ladha ya mboga yako.

Tovuti ya masuala ya mapishi, legit imeandika kuwa, maji ya limao na siki (vinegar) vinaweza pia kufanya kazi hiyo hiyo. Hivyo kazi ni kwako.

Unaweza kutofautisha nyama kwa rangi. Nyama iliyokoza ni ya mnyama mwenye umri mkubwa. Picha| mashed.

Fahamu juu ya uchaguzi wa nyama

Wataalamu wa nyama husema kila kiungo cha mwili wa mnyama kina utamu na wepesi wake kwenye kuiva.

Bila shaka ulishwahi kuingia buchani na ukasikia maneno kama nyama ya salala, mbavu, nundu na orodha inaendelea.

Kila kiungo cha nyama kina faa kwa pishi fulani.

Mfano mbavu kwa kuchoma na nundu kwa mishikaki.

Pia, kwa upande wa nyama kuiva haraka, ng’ombe mzee nyama yake itachukua muda mrefu zaidi kuliko ng’ombe kijana. 

Legit inaandika kuwa, nyama ngumu huwa na rangi iliyokoza zaidi.

Pia, inashauriwa kuweka chumvi mwishoni wakati nyama imeshaiva. Gazeti la The Independent limeandika kuweka chumvi kwenye yama ambayo bado haijaiva inafanya nyama hiyo kuwa ngumu.

Kwa leo wacha nikupe nafasi ya kupika nyama. Hadi wakati ujao, tuzungumzia majiko ya umeme ya kuchomea nyama.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa