Nyama ya kuku ni miongoni mwa vitoweo maarufu vinavyotumika kuandaa mapishi mbalimbali ikiwemo kuku choma, kuku wa kukaanga, kuku wa ndimu, kuku sekela na aina nyingine nyingi.
Licha ya kuwepo kwa mapishi ya lukuki ya kitoweo hicho bado una nafasi ya kuongeza ubunifu kwa kutumia aina mbalimbali za viungo ikiwemo bamia.
Kwa wapenzi wa bamia hapa ndio penyewe, unachotakiwa kufanya ni kuambatana nasi mpaka mwisho wa makala hii ili ujifunze jinsi ya kuandaa rosti kuku lilichonganywa na bamia.
Maandalizi
Maandalizi ya pishi hili yataanzia sokoni ambapo utanunua mahitaji yote utakayotumia ikiwemo kuku, bamia, kitunguu swaumu, nyanya ya kopo, kitunguu maji, mafuta ya kupikia, karoti, pilipili hoho na chumvi kiasi.
Baada ya kununua mahitaji yote, osha kuku na viungo vingine kisha vikate kate kwa saizi upendayo na uweke katika chombo kisafi.
Endelea na mapishi kwa kaanga kuku wako kwenye mafuta mpaka wabadilike na kuwa na rangi ya kahawia geuza upande wa pili nao uive kiasha utoe wachuje mafuta.
Bandika sufuria jikoni, weka mafuta na yapata moto weka vitunguu maji na upike kwa dakika tatu kisha weka kitunguu swaumu vilivyo sagwa, karoti na pilipili hoho na ukoroge kwa dakika tatu au nne.
Hatua hiyo ikikamilika weka nyanya ziache ziive kisha ongeza bamia, vipande vya kuku vilivyokaangwa, chumvi,maji kiasi pamoja na viungo vingine vya mchuzi kama unapendelea kisha ufunike viive.
Baada ya dakaika 10 hadi 15 bamia zitakuwa zimeiva na ukiridhishwa na kiwango cha mchuzi pishi lako litakuwa tayari kwa kula. Unaweza pia kuongeza nazi ili kufanya mchuzi uwe mzito na kuvutia zaidi.