Jinsi ya kupika samaki aina ya Nguruka 

Na Lucy Samson
29 Jan 2025
Samaki huyo anaweza kuchomwa na kusindikizwa na ugali pamoja na kachumbari au kupikwa rosti.
article
  • Nguruka anaweza kuchomwa na kusindikizwa na ugali pamoja na kachumbari.
  • Pia unaweza kuandaa rosti ambalo unaweza ukala na wali au chakula kingine.

Nguruka ani miongoni mwa aina za samaki zilizojizolea umaarufu katika mkoa wa Morogoro ambao wenyeji wake wanauita ‘mji kasoro bahari’.

Kwa wageni mkoani humo wanaweza kudhani  jina la samaki huyo ni kirefu cha samaki nguru ambaye mara nyingi huuzwa kwa vipande katika miji na maeneo ya pwani.

La hasha, nguruka ni tofauti na samaki nguru na utofauti wake upo kwenye maandalizi hadi muonekano wa nje ambapo samaki nguruka huwa wadogo wadogo wanaoandaliwa kwa mafuta ya mawese na chumvi nyingi wakati samaki aina ya nguru mara nyingi huuzwa wakiwa wamekatwa vipande.

Wenyeji wa Morogoro wanafahamu utamu wa samaki huyo hususan akichomwa na kusindikizwa na ugali pamoja na kachumbari.

Mbali na aina hiyo iliyozoleka jikopoint inakuletea maandalizi rahisi ya rosti la nguruka unaloweza kula pamoja na wali, chapati au aina nyingine ya msosi.

Rosti la nguruka hunoga kwa wali hususani ukiwa wali wa nazi. Iyawa/Instagram. cookhouse

Maandalizi

Kwa kuwa nguruka ni samaki mwenye chumvi hivyo hatua ya kwanza ni kuloweka katika maji ya moto kwa dakika kadhaa ili kupunguza chumvi iliyopo kisha unaweza kumtoa na kumuweka katika chombo kisafi kwa ajili ya mapishi.

Hatua hiyo pia itakusaidia kupunguza mafuta ya mawese yanayotumika kuhifadhia samaki huyo kama hupendelei.

Baada ya hapo utaendelea na maandalizi ya kawaida ambayo ni kumenya nyanya, vitunguu,nyanya chungu, kusaga karoti na kukuna nazi ili kutoa matui mawili.

Anza mapishi yako kwa kuwasha jiko, bandika sufuria na ikipata moto uweke mafuta kiasi ikifuatiwa na vitunguu ambavyo utavipika kwa dakika moja au mbili vikifuatiwa na nyanya chungu.

Hatua inayofuata ni kuweka nyanya na kuzifunika mpaka ziive kisha utaweka tui la pili utakaloliacha jikoni mpaka lichemke ikifuatiwa na nguruka na baadae tui zito la kwanza.

Ukifika hatua hii acha tui lichemke kisha uongeze chumvi (kama iliyopo haitoshi) pilipili hoho, karoti zilizosagwa na pilipili kama unatumia.

Acha vyote vichemke na kuiva vizuri na ukiridhika na kiwango cha mchuzi kilichobakia mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa