Wapenzi wa mboga za majani leo tumewafikia, tutajifunza kwa pamoja jinsi ya kuandaa mboga ya spinach iliyonakshiwa viungo mbalimbali ikiwemo karoti ambayo huongeza ladha na vitamini mwilini.
Inawezekana hupendi mboga za majani ila kwa aina hii ya mapishi hakika utaipenda na unaweza pia kuwaandalia watoto au wageni watakaokutembelea.
Mbali na ladha tamu Spinachi ina wingi wa vitamini A, K, C, B6 na potassium ambavyo Taasisi ya chakula na Lishe Tanzania (TFNC) inabainisha kuimarisha kinga mwili.
Namna ya kuandaa hatua kwa hatua
Hatua ya kwanza katika chombo kisafi chenye maji osha mboga za spinachi, karoti na kitunguu maji ili kuondoa mchanga na uchafu kwenye mboga.
Baada ya kuosha endelea kwa kukata mboga kwa kuzingatia muongozo wa uaandaaji chakula kama inavyoshauriwa na wataalamu kisha hamia kwenye karoti na vitunguu maji ambavyo utavikata katika vipande virefu vyembamba.
Maandalizi yakikamilika anza kwa kuwasha jiko na itapendeza zaidi ukitumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na jiko la umeme ambalo litaharakisha mapaishi na kutunza virutubisho vya mboga za majani.
Endelea na mapishi kwa kubandika sufuria na ikipata moto weka mafuta ya kupikia yakifuatiwa na kitunguu maji utakavyopika kwa dakika mbili hadi viwe na rangi ya kahawia.
Weka spinachi zilizokatwa katawa na kuoshwa vizuri ikifuatiwa na binzari, garam masala na uzifunike kwa dakika tatu kisha uendelee kwa kuweka karoti pamoja na chumvi na uzifunike kwa dakika nyingine nne ziive.
Hakikisha mboga zako hazikai kwa muda mrefu jikoni ili zisipoteze ladha na virutubisho vinavyohitajika, unaweza kuongeza nazi na pilipili kama unapendelea.
Mpaka hapo mboga ya spinachi ipo tayari kwa kuliwa na unaweza kuila kwa ugali, wali ama chapati.