Jinsi ya kupika supu ya samaki

Na Fatuma Hussein
20 Feb 2025
Supu hii sio tu ni tamu pia ina virutubisho muhimu kama protini,mafuta na vitamini A,na B.
article
  • Supu hii sio tu ni tamu pia ina virutubisho muhimu kama protini,mafuta na vitamini A,na B.
  • Unaweza kuandaa kwa ajili ya familia au biashara.

Supu ya samaki ni chakula chepesi lakini chenye nguvu, likichosheheni ladha tamu inayoweza kutumiwa na watu wa rika zote ikiwemo watoto, wanawake waliotoka kujifungua au wazee.

Pamoja na kutumiwa sana na makundi hayo, mlo huo pia una wingi wa virutubisho muhimu kama Protini , mafuta, madini ya chuma, vitamini A, vitamini B, kalsiamu, zinki, magnesiamu, fosforasi na  seleniumu kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) 

Faida hizo za kiafya hupoatikana kutokana na matumizi ya samaki na mboga mboga ikiwemo karoti, pilipili hoho zinazotumika kunogesha zaidi pishi hilo.

Supu ya samaki hutumiwa zaidi wakati wa kifungua kinywa asubuhi huku wengine wakiitumia jioni kama mlo wa usiku ikisindikizwa na vitafunwa kama chapati, maandazi au mikate.

Ikiwa unapenda supu ya samaki na haujui jinsi ya kuiandaa usiwaze, leo jiko point imekuletea maandalizi rahisi ya mlo huo kwa kutumia mahitaji machache yanayopatikana kwa urahisi nyumbani.

Namna ya kuandaa hatua kwa hatua

Hatua ya kwanza chukua samaki na uwasafishe vizuri hakikisha umewaosha na kuwatoa magamba kama wanayo.

Baada ya hapo chukua sufuria kubwa kishaa weka samaki muache akauke yale maji ya shombo kidogo ila kuwa makini asishikie kwenye sufuria.

Hatua inayofuata ni kuongeza  maji katika sufuria hiyo hiyo ikifuatiwa na mafuta ya kula vijiko viwili, itapendeza zaidi kama ukitumia mafuta ya zaituni, alizeti au karanga maana ndio mazuri kwa afya kisha acha ichemke.

Maji yakianza kuchemka, punguza moto na uache samaki waive kwa dakika 15 mpaka 20 ikifuatiwa na kitunguu, chumvi kiasi na karoti na uafunike viive.

Baada ya dakika tano ongeza limao na hoho ukipenda unaweza kuweka pilipili, mbogamboga kidogo kama kabichi, brokoli ama mchicha ili kuongeza ladha zaidi.

Ukimaliza hatua hizo zote supu yako ya samaki itakuwa tayari kwa kuliwa na unaweza kula kwa chapati, maandazi au ukaitumia yenyewe na mambo yakawa murua.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa