Jinsi ya kupika wali wa manjano wenye asili ya India

Na Lucy Samson
13 Oct 2023
Kutoka nchini India tunakuletea wali wa njano au ‘sweet turmeric rice na kutoka nchini Ujerumani tunakusogezea sosi ya nyama ya Ng’ombe( Beet stroganoff) mezani kwako upate kufurahia pamoja na uwapendao
article
  • Chakula hiki kinafaa zaidi kwa ajili ya wageni au familia
  • Kitasindikizwa na sosi ya nyama kutoka Ujerumani

Ni utamaduni wa kawaida uliozoleka kwa baadhi ya watu kuandaa chakula maalum kwa ajili ya wageni wanaowatembelea.

Hata hivyo, baadhi ya watu hupata shida kubuni aina mpya ya chakula wanachooweza kupika kwa ajili ya wageni, au wawapendao.

Ikiwa wewe ni miongoni mwa wahanga wa tatizo hilo, nikukaribishe katika makala hii ambapo tutajifunza mapishi ya chakula kutoka nchini Ujerumani na India.

Kutoka nchini India tunakuletea wali wa njano au ‘sweet turmeric rice na kutoka nchini Ujerumani tunakusogezea sosi ya nyama ya Ng’ombe( Beet stroganoff) mezani kwako upate kufurahia pamoja na uwapendao

Maandalizi ya msosi huu ni rahisi sana ikiwa utafuatana nami mwanzo mpaka mwisho wa kamala hii.

Miongoni mwa mahitaji yaliyotumika kupika wali wa manjano na sosi ya nyama.Picha|Frank William.

Sogea jikoni tupike

Anza kuandaa mahitaji utakayoyatumia katika pishi hili yaani mchele, nyama laini ya ng’ombe (fillets), njegere, mchicha, na nanasi kwa kuosha na kukakata.

Baada ya hapo weka kitunguu swaumu, tangawizi na limao kiasi kisha uiache kwa dakika 30 viungo vikolee kabla ya kuichemsha.

Baada ya muda huo kupita washa jiko bandika nyama funika ichemke kidogo bila kuweka maji kwa dakika tano au zaidi.

Kishakauka ongeza maji, ajinomoto ( kiungo cha kulainisha nyama), kitunguu maji, giligilani ya majani, pilipili manga, iriki na mdalasini, koroga na uache iive.

Wakati nyama inaiva unaweza kuanza kupika wali manjano, chemsha maji ya moto utakayoyatumia katika upishi wa wali.

Bandika sufuria, mimina mafuta kiasi alafu weka mchele uliouchambua na kuusafisha (unaweza kupika bila kuosha kama unapendelea) ongeza viungo kama mdalasini, manjano, pilipili manga,chumvi na binzari nyembamba kisha ukoroge viungo vichanganyike.

Dakika mbili hadi tatu zinatosha kuchanganya wali na viungo hivyo weka maji kiasi na ufunike uive kwa dakika 20 au zaidi ikiwa unatumia jiko la gesi.

Ukihisi wali wako umeanza kuiva ongeza mchicha uliokata kata na kuosha vizuri, njegere, karoti na vitunguu maji kisha ufunike kwa dakika tano ili mboga mboga ulizoweka ziive.

Baada ya dakika hizo kupita geuza, ongeza vipande vya nanasi kisha uufunkie jikoni kwa moto mdogo mddogo ili uendelee kuiva taratibu.

Ili chakula kikamilike (ballanced diet) ni lazima kuwepo matunda au saladi kama iliyopo katika chakula chetu.Picha|Daudi Mbapani.

Tuendelee na mapishi ya sosi ya nyama

Nyama ikishachemka epua, kumbuka nyama aina ya ‘fillet’ haichukui muda kuiva hivyo usiiache jikoni muda mrefu.

Katika sufuria safi mimina mafuta kiasi,yakipata moto weka vitunguu, karoti, hoho kisha koroga kwa dakika kadhaa na uongeze nyama.

Endelea kukoroga, ongeza soya sauce, chumvi kiasi, garam masala, manjano, giligilani ya majani, nyanya ya pakti, nyanya ya maji na vipande kadhaa vya nanasi kisha ufunike viive.

Viungo vikiiva, ongeza maji kidogo ili mboga yako iwe na mchuzi kiasi, ikichemka  mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa pamoja na wali wa manjano tuliouanda awali.

Ongeza juisi ya matunda, maji ya kutosha na saladi na mlo wako utakuwa umekamilika.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa