Kande za mahindi mabichi: Chakula bora kuimarisha afya yako

Na Mariam John
6 Jul 2022
Kande hizo ni za mahindi mabichi na maharage ambayo yanapikwa pamoja na viungo vingine ikiwemo nyanya, nazi, mafuta na kitunguu maji.
article
  • Unaweza kupika kwa kuchanganya na nafaka ikiwemo maharage.
  • Chakula hicho kinasaidia kuupatia nguvu mwili.

Mwanza. Mahindi mabichi ambayo yametoka kuvuna yanaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo mapishi.

Unaweza kutumia mahindi kupata chakula kwa kuyachoma, kuyachemsha au kuyamenya na ukapika kama kande zilizochanganywa na nafaka nyingine. 

Leo katika maujanja ya mapishi tunajikita katika uandaaji kande unazoweza kupika kwa kuchanganya na nafaka ikiwemo maharage, choroko au njugu.

Mahitaji
Pukuchua mahindi yako vikombe viwili au kimoja na nusu itategemea na aina ya familia uliyonayo. Pia andaa maharage kikombe kimoja cha chai, nyanya moja, kitunguu maji, kitunguu swaumu kama utapenda na mafuta kidogo ya kupikia kama kijiko kimoja cha chai.

Chemsha maharagwe yako hadi yaive, chemsha na mahindi pembeni nayo yaive kisha.

Baada ya mchakato huo, chukua sufuria lingine pembeni na uanze kuunga chakula chako pendwa upate ladha nzuri.

Weka kitunguu na nyanya kwenye mashine ya kusagia chakula kutengeneza rojo. Endapo hutatumia mashine, unaweza pia kukwangua au kukata vipande vidogo vidogo.

Bandika sufuria la kupikia kwenye moto wa wastani, weka maharage, rojo ya nyanya, kitunguu saumu, mafuta na kikombe kimoja cha maji. Kama mahindi yako siyo malaini sana weka maharagwe na mahindi pamoja. 

Changanya mchanganyiko huo kisha funika na mfuniko, acha iive taratibu kwa moto wa chini kwa dakika 20, endapo maji yatakauka, ongeza maji zaidi, hakikisha kila kitu kimeiva vizuri.


Baada ya maharage na mahindi kuiva vizuri ongeza tui la nazi, pika kwa dakika 5 nyingine ongeza chumvi ili kupata ladha.

Na sasa chakula chetu kitakuwa kimeiva tayari kupelekwa mezani kwa walaji.  Unaweza kutumia kinywaji chochote kwenye mlo wako huo; chai au juisi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa